Saturday, April 1, 2017

UHUSIANO WA SAUDIA NA SUDAN, HAKIKA AU MASLAHI YA MUDA?

Saudi Arabia inafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Sudan yajulikanayo kama 'Ngao ya Samawati -1' huku nchi hizo mbili zikijaribu kuimarisha uhusiano wao kutokana na vizingiti vya ndani ya nchi na kieneo.
Mazoezi hayo ya anga baina ya majeshi ya Sudan na Saudia yanayofanyika katika mipaka ya kaskazini mwa Sudan, yameanza Machi 29 na yataendelea hadi Aprili 12.
Uhusiano wa Sudan na Saudi Arabia umekuwa ukiimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Sudan ni kati ya nchi ambazo zinashiriki katika hujuma ya kinyama ya Saudia nchini Yemen. Pamoja na hayo, ushiriki wa Sudan katika muungano huo wa Saudia, sawa na ushiriki wa nchi zinginezo, ni wa kinembo tu na kwa ajili ya kupata misaada ya kifedha ya Saudia.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa Sudan na Saudia wamekuwa wakikutana kujadili uhusiano wa pande mbili katika sekta za kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Ingawa Sudan inataka misaada ya kifedha katika uhusiano wake na Saudia, lakini mkondo wa kuimarika uhusiano wao ni katika fremu ya Saudi Arabia kutaka kujipenyeza na kuwa na ushawishi barani Afrika. Ni kwa msingi huo ndio maana Rais Omar El Bashir wa Sudan hivi karibuni akatoa matamshi ya kustaajabisha kuwa eti usalama wa Saudia ni usalama wa Sudan!
Ndege ya kivita ya Saudia
Sababu kuu ya Saudia kukodolea macho ya tamaa nchi za Afrika ikiwemo Sudan ni matukio ya kasi Mashariki ya Kati ambayo hayaendi tena kwa maslahi ya watawala wa Riyadh. Wakuu wa Saudia wanaamini kuwa, hivi sasa uwezo na satwa yao iko katika mkondo wa kuporomoka katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa msingi huo,  Saudia sasa inataka kutumia uwezo wake wa kifedha ili kueneza ushawishi wake ya kisiasa barani Afrika na kupata waitifaki katika bara hilo. Kwa msingi huo,  Sudan imesema Saudia itawekeza dola bilioni 111 nchini Sudan na kwamba kiwango hicho cha uwekezaji kitaongozeka maradufu katika siku za usoni.
Wakati huo huo, Saudi Arabia kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika nchi za Kiarabu na Kiafrika inataka kutuma ujumbe huu kwa nchi zingine kuwa ina ushawishi mkubwa katika katika nchi za Kiafrika na Kiarabu.
Eneo la Hala'ib la Sudan kaskazini linalozozaniwa na Misri
Weledi wa mambo wanasema hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Saudia kufanya mazoezi ya kijeshi na Sudan, wakuu wa Riyadh wanataka kutuma ujumbe kwa nchi jirani ya Misri. Hii ni kwa sababu mazoezi hayo yanafanyika karibu na mpaka wa Sudan na Misri wakati uhusiano wa Misri na Saudia unaripotiwa kuvurugika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Nukta muhimu hapa ni kuwa, licha ya mazoezi hayo ya kijeshi, uhusiano wa Sudan na Saudia unaimarika kwa sababu ya matatizo yaliyoibuka hivi sasa katika nchi hizo mbili. Katika upande mmoja Saudia inashuhudia kufeli sera zake zisizo na busara Mashariki ya Kati huku serikali ya Omar El Bashir nayo ikikumbwa na matatizo mengie ya kiuchumi na hivyo kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment