Saturday, April 22, 2017

KOREA KASKAZINI: TUMEJIANDAA KUIKABILI MAREKANI NA HATUTISHIKI NA MELI ZAKE ZA KIVITA

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza utayarifu wake wa kukabiliana na hatua yoyote ya kichokozi ya Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini sambamba na kutangaza habari hiyo imesema kuwa, katika kufuatilia nyendo za Marekani, Pyongyang imejiandaa kukabiliana na chokochoko za Washington. Katika ripoti hiyo, Pyongyang imezungumzia hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kutuma meli zake za kivita katika maji ya Peninsula ya Korea na kuongeza kuwa, Pyongyang haitishiki na jambo hilo.
Kim Jong-un akiwa na makomando wa nchi yake
Kadhalika Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, hatua hizo za Marekani kamwe haziiogofyi nchi hiyo na kwamba jeshi lake linasubiri amri ya kukabiliana haraka na Marekani. Marekani ilituma meli zake za kivita katika Peninsula ya Korea baada ya kushtadi mgogoro baina yake na Korea Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo China na Korea Kaskazini zimesisitiza mara kadhaa kwamba, uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo, unatishia usalama wa nchi hizo sambamba na kusababisha kuibuka mashindano ya silaha katika eneo. Katika hatua nyingine, serikali ya Pyongyang imeionya China kwamba kuendelea vikwazo vya nchi hiyo dhidi yake, kutaharibu mahusiano ya nchi mbili.
Viongozi wa Uchina na Korea Kaskazini
Taarifa iliyotolewa na Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, kuendelea mwenendo huo wa vikwazo vya Uchina ni suala ambalo litakuwa na hatima mbaya katika mahusiano ya nchi hizo. Siku chache zilizopita, Beijing ilitangaza kusimamisha safari za ndege zake kwenda Korea Kaskazini huku ikisema kuwa, hatua hiyo haijatokana na sababu za kisiasa. Kabla ya hapo China ililalamikia hatua ya Pyongyang ya kufyatua kombora la balestiki kuelekea maji ya China na kukitaja kitendo hicho kuwa hatari. China na Korea Kaskazini zinafahamika kwa kuwa na mahusiano ya karibu kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment