Tuesday, April 18, 2017

KOREA KASKAZINI YALAANI MAREKANI KWA 'KUHUJUMU ' AMANI

Balozi wa Korea Kaskazini ameituhumu Marekani kuhujumu amani na utengamano katika Rasi ya Korea wakati mvutano ukishamiri katika eneo hilo. Akizungumza katika Umoja wa Mataifa Balozi Kim In-ryong alisisitiza kuwa Korea Kaskazini iko tayari kwa vita kamili na Marekani. Alisema mwenendo wa Marekani wa kutumia ubabe kuzivamia nchi huru na baadaye kudai inachangia katika kulinda amani ya dunia ni kukosa uwajibikaji. Korea Kaskazini ambayo hujulikana pia kama Jamhuri wa Kidemokrasia ya Watu wa Korea ilizidisha mvutano wa kikanda kwa kufanya jaribio jingine la kurusha kombora ambalo lilishindwa Jumapili. Wanadiplomasia kadhaa wa nchi hiyo wamesema nchi yao itaendelea kufanya majaribio mengine kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.

No comments:

Post a Comment