Wednesday, April 12, 2017

SUDAN YAKIRI KUUAWA WANAJESHI WAKE NCHINI YEMEN

Duru mbalimbali za kijeshi za Sudan zimekiri kuwa wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo wameuawa nchini Yemen.
Televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imezinukuu duru za jeshi la Sudan zinazohusika na vita vya Yemen zikikiri kuwa wanajeshi watano wa nchi hiyo wameuawaa katika mapigano na jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, afisa mmoja wa kijeshi wa Sudan ni miongoni mwa wanajeshi waliouawa huko Yemen. Wanajeshi wengine 22 wa Sudan wamejeruhiwa.
Rais Omar al Bashir wa Sudan

Mwezi Februari 2016, Saudi Arabia ilitumbukiza dola bilioni moja katika Benki Kuu ya Sudan na kufanikiwa kubadilisha msimamo wa Rais Omar al Bashir aliyekubali kushirikiana na Saudi Arabia katika uvamizi na mauaji ya raia wa Yemen. Hata hivyo fedha hizo ni kama rehani na amana, wakati wowote Saudia itakapozihitajia, lazima Sudan izirejeshe. Imechukuliwa hatua hiyo ili kumbana Rais Omar al Bashir asibadilishe msimamo wake.
Vile vile Saudi Arabia imewekeza katika miradi ya maji safi nchini Sudan katika hatua nyingine inayoonekana ni kuwapa hongo Wasudan.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa, mgogoro wa Yemen ambao ulishadidi kutokana na uvamizi wa Saudi Arabia mwaka 2015, umeshapelekea maelfu ya raia wa kawaida kuuawa na miundombinu kuharibiwa kabisa.

No comments:

Post a Comment