Duru za habari nchini Cameroon zimearifu kwamba, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram limetekeleza shambulio katika kijiji cha Mbreché, kaskazini mwa nchi hiyo na kuteka nyara wasichana kadhaa wenye umri wa miaka kati ya minane hadi 14.
Taarifa iliyotolewa na vyombo vya salama nchini Cameroon imesema kuwa, katika shambulizi hilo, wanachama wa kundi hilo la kigaidi wamesababisha hasara kubwa kwenye nyumba za kijiji hicho kilichoko karibu na mpaka wa pamoja na Nigeria. Hadi sasa hakujatolewa taarifa kamili juu ya kiwango cha hasara iliyosababishwa na hujuma hiyo.
Katika shambulizi lililofanywa siku chache zilizopita na kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram dhidi ya mji wa Kolofata, kaskazini mwa Cameroon, karibu watu 10 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa. Inafaa kuashiria kuwa, wanachama wa kundi hilo walivamia mji wa Kolofata mwezi Julai mwaka 2014 na tangu wakati huo wameendelea kuwepo mjini hapo. Utekaji nyara wanawake na wasichana kunakofanywa na wanachama wa kundi hilo la kigaidi kunajiri katika hali ambayo, hadi sasa serikali ya Nigeria bado inaendeleza juhudi za kuwakomboa wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara mwaka 2014.
Katika fremu hiyo, hivi karibuni jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa, jumla ya mateka 1,623 wamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Boko Haram katika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi katika jimbo la Borno na kwamba katika operesheni hizo magaidi 21 waliangamizwa.
No comments:
Post a Comment