Tuesday, June 27, 2017

PROPAGANDA ZA KITOTO ZA MAREKANI DHIDI YA SYRIA

Mapema jana asubuhi, Ikulu ya Marekani (White House) ilitoa tamko lisilo na mashiko ikidai kuwa serikali ya Syria ina nia ya kufanya shambulio la silaha za kemikali.
Katika tamko lake hilo, Ikulu ya Marekani imezungumzia matokeo ya shambulio ambalo hata halijafanyika na kudai kuwa: Eti Washington imegundua mpango wa serikali ya Syria wa kufanya shambulio la silaha za kemikali lenye nia ya kuua kwa umati raia wakiwemo watoto wadogo wasio na hatia. 
al Shairat, Syria

Marekani imedai pia kuwa, eti harakati za hivi sasa za serikali ya Syria zinafanana na zile za kabla ya shambulio la kemikali la rehe 4 Aprili 2017. White House imekumbushia shambulio la kemikali lililotokea katika eneo la Khan Sheikhun katika mkoa wa Idlib nchini Syria ambapo makumi ya watu waliuawa. Marekani na madola ya Magharibi yaliituhumu serikali ya Syria kuwa ilifanya shambulio hilo na hapo hapo Washington ikashambulia kambi ya jeshi la anga la Syria cha Shayrat katika mkoa wa Homs kwa makombora ya Tomahawk kabla ya hata kuthibitishwa iwapo ni kweli shambulio hilo lilitokea au la. Marekani ilifanya shambulizi hilo bila ya hata idhini ya Umoja wa Mataifa na licha ya kwamba mwaka 2014, Umoja wa Mataifa uliwatangazia walimwengu wote kuwa Syria haina tena silaha za kemikali. 
Seymour Hersh ni mwandishi wa habari maarufu wa nchini Marekani. Amesema kuhusiana na jambo hilo kwamba, kinyume kabisa na madai mapya ya wanasiasa wa Ikulu ya Marekani (White House) wanaodai kuwa serikali ya Syria inajiandaa kufanya shambulizi la kemikali; kwa upande wao, maafisa wa kijeshi wa Marekani wanasema hawana taarifa zozote za jambo hilo. Seymour Hersh amejibu madai hayo mapya ya serikali ya Marekani dhidi ya Syria kwa kusema: Maafisa wa kijeshi wa Marekani wamesema kwamba, hawana taarifa yoyote ya kujiandaa Damascus kufanya shambulio la kemikali.

Madai ya wanasiasa wa Marekani ya kwamba serikali ya Syria inajiandaa kufanya shambulio la kemikali yametolewa katika hali ambayo, duru mbalimbali za Marekani ikiwemo taasisi ya nchi hiyo ya utafiti kuhusu magaidi wa Daesh inayojulikana kwa jina la IHS imetangaza mara nyingi kuwa, tangu mwaka 2014 hadi hivi sasa, genge la kigaidi la Daesh (ISIS) limefanya makumi ya mashambulio ya kemikali katika nchi za Syria na Iraq. Wimbi la propaganda mpya za Marekani dhidi ya Damascus limezushwa katika hali ambayo jeshi Syria na vikosi vya kujitolea vya wananchi, linazidi kupata ushindi katika medani za kupambana na magenge ya kigaidi nchini humo. Katika wiki za hivi karibuni, maeneo mengi ya Syria yamekombolewa kutoka kwenye makucha ya magenge ya kigaidi yanayopata misaada ya kila namna kutoka nje ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia hayo, jeshi la Syria halina haja yoyote ya kutumia silaha za kemikali kwani linazidi kupata ushindi katika medani za mapambano. Pande ambazo zina uwezekano mkubwa wa kufanya mashambulizi ya kemikali ni zile zinazozidi kushindwa na kupoteza maeneo ziliyokuwa zinayashikilia. Hakuna anayepinga kuwa, magenge ya kigaidi nchini Syria, hayasiti hata kidogo kufanya jinai yoyote ile. Hivyo kutumia magenge hayo ya kigaidi, silaha za kemikali yalizopewa na nchi za Magharibi, ni jambo rahisi sana. 
Serikali ya Syria imekumbwa na wimbi jipya la propaganda za kitoto za Marekani katika hali ambayo, tarehe 27 Septemba, 2017, Syria ilikabidhi kwa Umoja wa Mataifa silaha zake zote za kemikali kwa mujibu wa azimio nambari 2118 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na umoja huo ukaishukuru rasmi serikali ya Syria kwa ushirikiano wake huo mzuri. 
Rais Bashar al Assad wa Syria akikagua wanajeshi walioko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magaidi

Kwa kweli si jambo la kushanga kuiona Marekani na waungaji mkono wengine wa makundi ya kigaidi, wakiyakingia kifua magenge hayo ya kikatili kwa njia yoyote ile, ikiwa ni pamoja na kuisakama kwa kila aina ya propaganda serikali halali ya Syria. Hii pia si mara ya kwanza kwa waungaji mkono hao wa magaidi, kuyaunga mkono magenge hayo ya wakufurishaji kwa kila aina ya uungaji mkono, hasa pale wanapoona yameelemewa na mashambulio ya ukombozi wa ardhi ya Syria yanayoendeshwa na serikali ya Rais Bashar al Assad na waitifaki wake. Tusisahau pia kuwa, hivi karibuni, muungano unaoongozwa na  Marekani wa eti kupambana na ISIS umekuwa ukifanya mauaji makubwa ya raia huko Syria na Iraq. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, propaganda mpya za kitoto za Marekani dhidi ya Syria zina mfungamano wa moja kwa moja na njama za Marekani za kuficha jinai zake dhidi ya wananchi wa Syria. 

No comments:

Post a Comment