Thursday, July 6, 2017

WATU 80 WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA BARABARANIJAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Ajali ya lori moja la mizigo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR imesababisha vifo vya zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa ni wachuuzi waliokuwa wakielekea sokoni mjini Bambari.
Duru za madaktari zinasema kuwa, lori hilo lilipata ajali likiwa limepakia watu na mizigo kupita kiasi na kwamba, ajali hiyo imetokea yapata kilomita 10 hivi nje ya mji wa Bambari.
Wafanyabiashara hao wakiwa na bidhaa zao za biashara walikuwa wakielekea katika soko moja la kila wiki katika kijiji cha Maloum. Taarifa zaidi zinasema kuwa, zaidi ya watu 80 wameaga dunia kufuatia ajali hiyo huku wengine zaidi ya 72 wakijeruhiwa.
Mashuhuda wanasema kuwa, lori hilo lilikuwa limebeba watu wengi na kupakia mizigo kupindukia lilipata ajali  na kupinduka huku likiendeshwa kwa mwendo wa kasi.
Kawaida malori katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hupakia watu na mizigo namna hii
Ripoti zinaonyesha kuwa, kumekuwa kukitokea ajali kama hizo katika maeneo ya katikati na magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati huku chanzo cha ajali hizo kikitajwa kuwa ni ukiukaji wa sheria za barabarani.
Polisi ya usalama barabarani nchini humo inalaumiwa kutokana nja kutowachukulia hatua kali madereva wasioheshimu sheria za barabarani.
Baadhi ya duru zinasema kuwa, kikosi cha usalama barabarani kimekuwa kikipokea rushwa na hivyo kufumbia macho makosa ya madereva hasa ya mwendo wa kasi na kupakia abiria na mizigo kupita kiasi.

No comments:

Post a Comment