Tuesday, June 27, 2017

IRAN YALAANI UAMUZI WA MAHAKAMA KUU YA MAREKANI DHIDI YA WAISLAMU

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Marekani dhidi ya Waislamu na kusema kuwa, kutokana na mitazamo yake finyu ya kibiashara, Washington imefumbia jicho wasababishaji halisi wa ugaidi nchini Marekani na kutoa ujumbe usiofaa.
Bahram Qassemi amesema kuwa, uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Marekani dhidi ya Waislamu ni kielelezo cha mienendo ya kibaguzi ya serikali ya Washingon dhidi ya Waislamu na mtazamo usio wa kiadilifu kuhusu wafuasi wa dini hiyo. 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, mtazamo wa watawala wa Marekani kuhusu Waislamu wanaofanya safari au wanaoishi nchini Marekani daima umekuwa mbaya, wa dharau na kuwadhalilisha wafuasi wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu ambao kwa mujibu wa ushahidi wa historia wamekuwa wakiheshimu sheria, kuishi kwa amani na kujiehpusha na vitendo vya utumiaji mabavu na misimamo mikali.
Maandamano ya kupinga amri ya Trump, Marekani
Mahakama Kuu ya Marekani Jumatatu iliyopita iliiruhusu serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutekeleza sehemu ya amri ya kuwazuia Waislamu wa nchi kadhaa kuingia katika ardhi ya nchi hiyo. 
Amri hiyo ya Trump haikuwahusisha raia kutoka nchi kama Saudi Arabia na washirika wake ambazo ndiyo waleaji na waungaji mkono wa makundi ya kigaidi. 

No comments:

Post a Comment