Friday, June 9, 2017

WATU 39 WAUAWA KATIKA MASHAMBULIO YA MABOMU YA MAGAIDI WA DAESH IRAQ

Kwa akali watu 39 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya mabomu yaliyofanywa hii leo na kundi la kigaidi la Daesh katika miji ya Babil na Karbala nchini Iraq.
Vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza kuwa, watu wasiopungua 30 wameuawa katika shambulio la kwanza katika mji wa Babil ambapo mtu aliyekuwa amejifunga mabomu alijiripua katikati ya watu. Taarifa zaidi zinasema kuwa, watu 33 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kujitolea muhanga huku hali za baadhi ya majeruhi zikiripotiwa kuwa mbaya.
Mlipuko huo ulitokea katika mlango wa kuingia katika soko la eneo la al-Musayyib na kwamba, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya wahanga wa shambulio hilo la kigaidi. Taarifa za awali zinasema, mwanamke mmoja ndiye aliyetekeleza shambulio hilo kwa kujiripua katika mji huo ambao wakazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Wanachama wa kundi la kigaidi al Daesh nchini Iraq
Aidha katika tukio jengine watu wengine 9 wanaripotiwa kufariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya mtu mmoja kujiripua ndani ya kituo cha mabasi ya mji wa Karbala.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na mashambulio ya leo ya kigaidi nchini Iraq.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, raia 354 wameuawa nchini Iraq na wengine 470 kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yaliyofanywa na makundi ya kigaidi.

No comments:

Post a Comment