Mgogoro wa kidiplomasia ulioibuka kati ya Saudi Arabia ikishirikiana na nchi kadhaa za Kiarabu dhidi ya Qatar unaonekana kuchukua sura mpya baada ya watawala wa Aal Saud kuwazuia raia wa Qatar kuingia katika msikiti wa Makka.
Ripoti zinasema kuwa, baada ya kuzuka mgogoro huo raia wa Qatar wamekuwa wakizuiwa kuingia katika Masjid al-Haram.
Gazeti la al-Sharq limemnukuu afisa mmoja wa kamati ya taifa ya haki za binadamu ya Qatar akitangaza kuwa, raia wa nchi hiyo wamezuiwa na Saudia kuingia katika msikiti wa Makka. Aidha vyombo vya usalama vya Saudia vimewataka raia hao kuondoka nchini humo mara moja.
Ali bin Samikh Al Marri, Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar amelaani vikali hatua hiyo ya Saudia ya kuingiza masuala ya kisiasa katika ibada na kubainisha kwamba, hatua iliyochukuliwa na baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuiwekea vikwazo Qatar ni jinai ya kimataifa.
Ameongeza kuwa, kamati yao imeshapokea mashtaka 700 ya raia wa nchi hiyo waliodhurika na mzingiro wa Saudia na washirika wake dhidi ya Qatar.
Siku chache zilizopita nchi za Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar na kuzuia safari za anga, nchi kavu na baharini kuelekea katika nchi hiyo. Nchi nyingine kadhaa ambazo ni vibaraka wa Saudia nazo zimejiunga na nchi hizo.
Serikali ya Qatar imetangaza kuwa, Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu zinataka kuiweka nchi hiyo chini ya udhibiti wao suala ambalo linakiuka kikamilifu haki ya kujitawala na kusisitiza kuwa, jambo hilo kamwe haliwezi kukubalika.
No comments:
Post a Comment