Sunday, June 4, 2017

SERIKALI YA CHINA YAWALAZIMISHA WAISLAMU KUBADILI DINI MAJINA YA WATOTO WAO KWA MADAI YA KUPAMBANA NA MISIMAMO MIKALI

Kutokana na mashinikizo ya serikali ya eneo la Xinjiang nchini China kuwalenga Waislamu wa jimbo hilo la magharibi mwa nchi hiyo, wazazi Waislamu wanalazimika kubadilisha majina ya watoto wao walio na umri wa chini ya miaka 16 na kuwaita majina mengine yasiyo ya kidini.
Gazeti la Guardian limeandika kuwa, serikali ya kieneo tawi la chama cha Ukomunisti katika jimbo la Xinjiang nchini China, limepiga marufuku majina 15 ya Kiislamu kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 katika eneo hilo ambapo baadhi ya majina hayo ni 'Jihadi' 'Imamu' 'Hajj' 'Qur'an' 'Makkah' 'Madina' na 'Arafah.'
Jamii ya Waislamu nchini China
Katika mwezi huu wa Ramadhani viongozi wa serikali ya jimbo hilo wameziamuru familia za Kiislamu ambazo zina watoto walio na umri chini ya miaka 16 wenye majina miongoni kati ya 15 yaliyotajwa kwamba, ni lazima wawabadili watoto wao majina hayo. Hii ni katika hali ambayo mwezi Aprili mwaka huu, viongozi wa eneo hilo pia walitangaza marufuku ya kuwaita watoto wachanga majina ya Kiislamu huku marufuku hiyo ikipanua wigo wake hadi kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 ndani ya mwezi huu wa Ramadhani. Jamii ya Waislamu wa jimbo la Xinjiang inaundwa na watu wa kabila la Igor lenye asili ya Uturuki.
Watoto wa Kiislamu walio chini ya umri wa miaka 16 wakijifundisha Uislamu
Viongozi wa eneo hilo wanadai kuwa kutokana na wasi wasi walionao wa kupenya na kupanuka kwa wimbi la makundi ya kufurutu ada na katika kupambana na wimbi hilo, wameanzisha utekelezaji wa sheria kali jimboni hapo. Katika hatua ya awali ya kuweka sheria kali, bunge la eneo hilo limepitisha vipengee 15 vya sheria ambavyo kwa mujibu wake serikali ya Xinjiang itaanza kukabiliana na athari au alama zozote za Kiislamu ambazo kwa mujibu wa serikali hiyo, ni chanzo cha kuibuka misimamo mikali.
Jamii ya Waislamu ikiwa inakabiliwa na mashiunikizo ya askari katika mji wa Xinjiang
Itafaa kuashiria kuwa, tangu wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na idadi kadhaa ya magaidi wa kundi la harakati ya Turkestan, mashariki mwa China walipotoa vitisho vya kutekeleza mashambulio ya uharibifu eneo tajwa, serikali ya nchi hiyo ilituma zaidi ya maafisa usalama laki mbili eneo hilo. Hayo yanajiri katika hali ambayo kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa na asasi mbalimbali za kimataifa, kinyume na madai ya baadhi ya mataifa hususan ya Magharibi katika kuuhusisha Uislamu na ugaidi, wafuasi wa dini hiyo ya mbinguni ndio wahanga wakubwa wa jinai na mashambulizi ya magenge ya kigaidi.
Jamii ya Waislamu nchini China

No comments:

Post a Comment