Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anakabiliwa na msururu wa ukosoaji baada ya kampeni ya uchaguzi iliyoshindwa na kusababisha kupungukiwa na wingi katika bunge na anatarajia kuwania kulinda nafasi yake ya uongozi
Wakati akipambana kulinda nafasi yake ya uongozi lakini dakika zinayoyoma kuelekea kuanza mazungumzo ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Kamari aliyocheza May kwamba angeweza kutumia mapenzi ya watu wa Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya na kile kilichoonekana kuwa ni udhaifu wa chama cha upinzani cha Labour ilimrudia mwenyewe siku ya Alhamis wakati wapiga kura walipomuondolea wingi wake katika bunge.
Matokeo hayo ya kushangaza, ambayo yamesababisha sarafu ya pauni kuporomoka thamani, yamemlazimisha May kuunda serikali yenye wingi mdogo, na kumuacha kutegemea kundi dogo la wabunge wa Ireland ya kaskazini, ikiwa ni siku tisa tu kabal ya Uingereza kuanza majadiliano ya kupata makubaliano ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Vyombo vya habari vya Uingereza ambavyo kwa kawaida vina msimamo wa siasa za mrengo wa kulia vimemrarua May kuhusiana na matokeo ya uchaguzi, vikihoji iwapo ataweza kuendelea kubaki madarakani baada ya matokeo ambayo yanamuweka katika hali ya kutegemea kuyaunganisha makundi hasimu ndani ya chama chake ili kuweza kufanikisha Brexit.
"May anatumbua macho katika anga tupu," limeandika gazeti la Jumamosi la The Times wakati Daily Mail limeandika "Wahafidhina wamgeukia Theresa".
Gazeti la Telegraph limeandika wahafidhina waandamizi ikiwa ni pamoja na waziri wa mambo ya kigeni Boris Johnson , waziri wa mambo ya ndani Amber Rudd na waziri wa Brexit David Davis wanaangalia uwezekano iwapo wamuondoe madarakani.
May bado akakamaa
"Wakati nikitafakari kuhusiana na matokeo nitatafakari kuhusu kile tunachotakiwa kufanya hapo baadaye ili kukipeleka chama mbele," May amesema jana Ijumaa katika taarifa iliyotolewa katika televisheni.
Gazeti linalouzwa kwa wingi nchini Uingereza la Sun limesema wanachama waandamizi wa chama chake wameapa kumuondoa madarakani, lakini watasubiri kwa takriban miezi sita kwasababu wanawasi wasi kwamba mvutano wa kuwania uongozi kwa hivi sasa kunaweza kumuingiza madarakani kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn.
"Theresa May bila shaka ni kiongozi imara ambaye tunaye hivi sasa ," David Davis , waziri wa Brexit, ameliambia shirika la habari la BBC. Amesema kuwa itakuwa vigumu kutabiri iwapo bado atakuwa waziri mkuu mwishoni mwa mwaka huu.
Wabunge kadhaa walidai kujiuzulu kwa washauri wa ngazi ya juu wa May, ambao wamekuwa wakilaumiwa kwa sera mbovu kuwafanya wazee kulipa fedha zaidi kwa ajili ya matunzo yao na kampeni iliyoonekana kuwa iko mbali mno na watu wa kawaida na inayolenga mno kuwashambulia wapinzani wao.
Baada ya kuthibitisha jana Ijumaa (09.06.2017) kwamba mawaziri wake wa juu wataendelea na nyadhifa zao , ikiwa ni pamoja na waziri wa fedha Philip hammond , May anatarajiwa kuendelea kuliteua baraza lake la mawaziri ambalo litafanya moja kati ya majadiliano magumu kabisa katika historia ya Uingereza.
Mazungumzo kuanza kama yalivyopangwa
May amesema mazungumzo ya Brexit yataanza rasmi Juni 19 kama ilivyopangwa, siku hiyo hiyo ambayo bunge litafunguliwa rasmi. Lakini matokeo ya uchaguzi yana maana haiko wazi iwapo mpango wake kuitoa Uingereza kutoka katika soko la pamoja na Umoja wa Ulaya pamoja na umoja wa forodha unaweza pia kuendelea.
Wanasiasa wa Uingereza, ikiwa ni pamoja na wa chama cha May binafsi, wanatofautiana kwa kiasi kikubwa kuhusiana na kile wanachotaka kutoka katika mchakato wa majadiliano ya Brexit.
Iwapo atafanikiwa kufikisha mwisho wa uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ambapo asilimia 52 ya Waingereza walitaka mwaka jana, ni lazima atafute njia kuweza kupata uungwaji kamili mkono wa chama chake kwasababu atahitaji kura zao kuweza kupitisha sheria inayotayarisha uidhinishaji wa hatua hiyo ya kujitoa.
May pia atahitaji uungwaji mkono wa wahafidhina wanaopendelea masuala ya kijamii, chama cha siasa za kizalendo cha Democratic Unionist kinachopendelea kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (DUP) ambacho kimeshinda viti 10 katika Ireland ya kaskazini.
No comments:
Post a Comment