Friday, July 28, 2017

MAREKANI YAIWEKEA TENA VIKWAZO IRAN

Marekani imeendeleza uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuziwekea vikwazo taasisi 6 za Kiirani.
Wizara ya Fedha ya Marekani usiku wa kuamkia leo imeziwekea vikwazo taasisi hizo sita za Kiirani kwa kisingizio cha majaribio yaliyofanywa juzi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya roketi la kutuma satalaiti angani la Simorgh ambayo inahusiana kikamilifu na masuala ya kielimu na kisayansi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani imesema kuwa: Mali na milki za taasisi hizo sita za Iran katika ardhi ya Marekani zinazuiliwa, na taasisi za fedha za kigeni zinazuiwa kufanya muamala wowote na taasisi hizo.
Roketi la kubeba satalaiti angani la Simorgh lilizinduliwa Alkhamisi iliyopita kwa mafanikio katika Kituo cha Masuala ya Anga cha Imam Khomeini. Roketi hilo lina uwezo wa kupeleka angani satalaiti yenye uzito wa kilo 250 umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini. 
Uzinduzi wa roketi la Simorgh, Iran
Siku chache zilizopita pia Kongresi ya Marekani ilipasisha mpango wa vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile tarehe 18 mwezi huu wa Julai Wizara ya Fedha ya Marekani iliwawekea vikwazo watu na taasisi 18 za Iran na nchi za kigeni kwa kutumia visingizio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na uhusiano na miradi ya kutengeneza makombora ya Iran. 
Tangu iliposhika madaraka nchini Marekani, Serikali ya Donald Trump imezidisha uhasama na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

No comments:

Post a Comment