Thursday, July 6, 2017

MAGENDO YA MIHADARATIM TATIZO LISILO NA UFUMBUZI

Ongezeko la uzalishaji wa mihadarati na magendo ya madawa ya kulevya linaonekana kuitia wasi wasi dunia nzima, hata hivyo kile kinachopelekea ongezeko hilo na kulifanya jambo hilo kuwa tatizo lisilo na mwisho, ndicho chenye kutia wasi wasi zaidi.
Suala hilo ndilo lilikuwa nukta kuu iliyojadiliwa katika kongamano lililofanyika siku ya Jumanne ya tarehe 4 Julai mwaka huu hapa mjini Tehran, kwa mnasaba wa siku ya kimataifa ya kupambana na madawa ya kulevya. Katika kongamano hilo, Ali Larijani, Spika wa Majlis ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge la Iran, alisema: "Magendo ya madawa ya kulevya yameangamiza maisha ya watu wengi, na kusababisha matatizo makubwa kifamilia na kijamii. Alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya juhudi kubwa za kupambana na tatizo hilo, hivyo nchi nyingine nazo zinatakiwa ziwe na fikra moja kuhusiana na suala hilo. Kwani si sahihi gharama zote za kupambana na madawa ya kulevya zibebwe na Tehran peke yake." Mwisho wa kunukuu.
Askari wa Marekani katika moja ya mashamba ya mipopi inayozalisha mihadarati nchini Afghanistan
Hivi sasa na kwa mujibu wa makadirio ya dunia, ugaidi na uzalishaji madawa ya kulevya, ni mambo mawili yanayohesabiwa kuwa hatari kubwa kwa usalama wa taifa kieneo na kimataifa. Afghanistan ambayo ina mpaka mkubwa na Iran inahesabika kuwa chimbuko la uzalishaji wa madawa ya kulevya. Imepita miaka 16 sasa tangu Wamarekani walipoivamia nchi hiyo hapo mwaka 2001 kwa madai ya kile walichokisema kuwa ni kupambana na madawa ya kulevya na ugaidi. Katika kipindi chote hicho, askari wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na hasa hasa askari wa Uingereza, ambayo ina jukumu la kupambana na madawa ya kulevya nchini Afghanistan, hawajaweza kufikia mafanikio yoyote yale, kama ambavyo pia hawajapata maendeleo yoyote hata katika uga wa kupambana na ugaidi na harakati za makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka nchini humo.
Askari wa nchi za Asia wakiwa katika kiwanda cha kutengeneza madawa ya kulevya
Suala la kutia wasi wasi mkubwa katika uwanja huo ni kwamba, magendo ya madawa ya kulevya yamegeuka kuwa sehemu ya chanzo cha kifedha cha makundi ya kigaidi, fedha ambazo baadaye hutumiwa kuathiri usalama wa nchi za eneo hili zima na duniani kiujumla. Andrei Kazantsev, mchambuzi wa masuala ya kimataifa wa nchini Russia anasema: "Hali ya Afghanistan imekuwa na taathira kubwa kwa usalama wa nchi za Asia ya Kati. Kwa ujumla ni kwamba kadri inavyoendelea kuwa tishio kwa usalama wa eneo hilo, ndivyo pia huathiri usalama wa Russia." Mwisho wa kunukuu. Katika hilo kunaibuka swali kwamba, hivi juhudi nchi kadhaa za eneo ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na madawa ya kulevya, zinaweza kuwa na taathira inayotakiwa? Na je, ni kweli nchi zinazounga mkono ugaidi zina azma ya dhati ya kupambana na madawa ya kulevya. Ukweli wa kushtusha ni huu kwamba, hadi sasa takwimu zinaonyesha kwamba, watu milioni 10 wanajishughulisha na magendo ya madawa ya kulevya duniani, ambapo pesa zinazotokana na biashara hiyo zinafikia kiasi cha Dola Bilioni 1500 kwa mwaka.
Raia wa Afghanistan akiendelea kuhudumia shamba la madawa ya kulevya
Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa, mwaka jana 2016 uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini Afghanistan ulifikia tani 5600, ambapo karibu asilimia 35 ya madawa hayo yalivushwa na wafanya magendo hao kupitia mipaka ya Iran kwenda nchi nyingine. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa katika mstari wa mbele wa kupambana na madawa ya kulevya duniani, imeshapoteza zaidi ya askari 3500 waliouawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 10 kujeruhiwa katika mapambano na wafanya magendo ya madawa hayo ya kulevya. Katika kongamano jingine la kimataifa la kupambana na madawa ya kulevya lililofanyika mwaka huu mjini Tehran, Salamat Azimi, Waziri wa Kupambana na Madawa ya Kulevya wa Afghanistan sambamba na kuipongeza sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na juhudi zake kubwa za kukabiliana na janga hilo, alisema: "Tunataraji kuziona nchi majirani na Afghanistan zitatekeleza ahadi zao za kufunga mipaka yao na kupambana na wafanya magendo ya madawa ya kulevya kama inavyofanya Iran ya Kiislamu." Mwisho wa kunukuu.
Mamilioni ya Dola za madawa ya kulevya yaliyonaswa
Inafaa kuashiria kuwa, uzalishaji wa madawa ya kuvya nchini Afghanistan ni tishio ambalo si tu linahatarisha usalama wa eneo hili, bali ni hatari kubwa kwa usalama wa ulimwengu mzima. Na katika kudhamini usalama wa dunia kutokana na uzalishaji wa hatari hiyo nchini Afghanistan, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza nguvukazi nyingi kama alivyosema Spika wa Majlis ya Ushauri kwamba: "Hakuna irada ya kimataifa na ya kivitendo vya kupambana na mihadarati. Hivyo isitarajiwe kuwa Iran itakuwa tayari kugharamika peke yake katika mapambano ya madawa ya kulevya."

No comments:

Post a Comment