Mgogoro mwingine wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda unanukia. Hii ni baada ya makumi ya wahamiaji haramu raia wa Uganda kukamatwa na maafisa wa polisi wa Kenya katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Wambua Katiithi, Kamanda Mkuu wa Polisi katika mji wa Bumula, kaunti ya Busia amesema wahajiri haramu 53 wa Uganda wamekatwa wakiwa hawana vyeti vinavyohitajika vya usafiri, wakiwa njiani kuelekea mjini Nairobi kwa kutumia usafiri wa basi.
Tukio hilo lilifanyika hapo jana, ikiwa ni chini ya masaa 24 baada ya polisi ya Uganda kuwatia mbaroni askari polisi watatu wa Kenya na wavuvi kadhaa kati ya visiwa vya Mageta na Hama katika Ziwa Victoria.
Kenya na Uganda zimekuwa zikivutana kwa miaka kadhaa sasa kuhusu masuala kadha wa kadha na haswa umiliki wa kisiwa cha Migingo, kilichoko katika mpaka wa nchi mbili hizo za Afrika Mashariki.
Mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kisiwa cha Migingo katika Ziwa Victoria ni milki ya Kenya.
Mgogoro wa kisiwa cha Migingo ulianza mwaka 2008 baada ya wanajeshi wa Uganda kukivamia na kuwatimua Wakenya ingawa kimekuwa kikitambuliwa kuwa ni milki ya Kenya.
Makubaliano ya awali kati ya Kenya na Uganda kuhusu kisiwa hiki yalifanyika 2016, na kwa sasa maafisa wa usalama kutoka nchi zote mbili wanalinda doria katika kisiwa hicho.
Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un wamekubaliana kuondoa kabisa silaha za kinyuklia katika rasi ya Korea katika makubaliano ya pamoja ya kihistoria.
Viongozi hao walikamilisha siku ya kihistoria ambayo ilishuhudia viongozi hao wawili wakikutana kwa mara ya kwanza kabisa.
Katika mkutano huo Trump ameahidi kuipatia Korea kaskazini uhakikisho wa usalama wake pamoja na kutangaza katika mkutano na waandishi habari baadaye kwamba Marekani na Korea kusini zitaacha luteka ya pamoja ya kijeshi kama Korea kaskazini inavyodai.
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un (kushoto) na rais wa Marekani Donald Trump wakipeana mikoni
Katika waraka wenye vipengee vinne, Marekani na Korea kaskazini zimeazimia kuweka uhusiano mpya kati ya nchi hizo mbili, kujenga utawala imara na endelevu kuelekea amani akisisitiza azimio la Panmunjeom kutoka Aprili 27.
Katika mkutano na waandishi habari leo rais Donald Trump wa Marekani amesema kwamba jeshi la Marekani litaacha kufanya mazowezi ya pamoja na Korea kusini yakiilenga Korea kaskazini, akisema yanaongeza hali ya wasi wasi na kuyasitisha kutasaidia kuhifadhi fedha nyingi zinazotumika katika mazowezi hayo. Pia amesema atamwalika kiongozi wa Korea kaskazini katika ikulu ya marekani White house na kwamba binafsi angependa kutembelea mji mkuu wa Korea kaskazini Pyongyang.
Nchi hizo mbili hufanya mazowezi ya kijeshi kila mwaka ambayo yanaikera Korea kaskazini , ambayo imekuwa kwa muda mrefu ikidai kusitishwa kwa mazowezi hayo na mara nyingi hujibu kwa kuchukua hatua zake, na kusababisha kuongezeka kwa hali ya wasi wasi.
Rais Trump akionesha waraka uliotiwa saini baina yake na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un
Kim amshukuru Trump
Wakati wa kutia saini makubaliano hayo kati ya Trump na Kim leo asubuhi, rais Trump alisema pande zote mbili zimefurahi kutia saini makubaliano hayo.
"Tunatia saini waraka muhimu sana, waraka ambao una maelezo mapana. na tutajadili hili kwa kina. Kwa hivi sasa naamini mtapata nakala kwa niaba ya mwenyekiti Kim na mimi. Na wote tunafahari kubwa kutia saini waraka huu. Asante."
Kwa upande wake kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un alimshukuru rais Trump kwa kukubali kufanyika mkutano huo.
"Leo tulikuwa na mkutano wa kihistoria na kuamua kuacha nyuma yaliyopita. Na tuko tayari kutia saini waraka huu wa kihistoria. Dunia itaona mabadiliko makubwa. Napenda kueleza shukurani zangu kwa rais Trump kwa kufanikisha mkutano huu. Asante.
Kuhusu vikwazo dhidi ya Korea kaskazini rais Trump amesema kwa hivi sasa vikwazo hivyo vitaendelea , lakini anaangalia uwezekano wa kuviondoa.
Rais Trump akiwa katika mkutano na waandishi habari baada ya kutia saini makubaliano na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un
Rais wa Marekani amesema pia kwamba kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un ana nia thabiti ya kuharibu kabisa maeneo ambayo nchi hiyo inafanyia majaribio silaha zake.
Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenzake wa Malaysia mahathir Mohammed wamekubaliana leo kufanyakazi kwa pamoja kupambana na mipango ya kinyuklia na makombora ya Korea kaskazini. Viongozi hao wamesema wanataka kutuma ujumbe mkali kwa Korea kaskazini kuhusu suala hilo. Waliysema hayo katika mkutano na waandishi habari kufuatia mkutano wao mjini Tokyo
Magazeti ya Ujerumani yamemtaja Rais Donald Trump wa Marekani kuwa ni mtu asiyejua mipaka yake wala asiye na mantiki na yamezitaka nchi zote za Ulaya kuacha kumfuata kiongozi huyo.
Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung limeripoti kuwa, kila mtu aliyekuwa anaamini kuwa Rais wa Marekani ni mtu mwenye mantiki na anayetilia maanani uhakika wa mambo anapaswa kuzika matumaini hayo kwa sababu kuwepo kwa mtu huyo asiye na adabu na mbumbavu hakuifanyi dunia kuwa sehemu bora na yenye amani zaidi.
Gazeti hilo la Ujerumani limeongeza kuwa: Trump anaendelea kuzitishia nchi nyingine kwa kutumia mabavu na silaha ya uchumi, na suala hilo ni hatari sana kwa Ujerumani.
Süddeutsche Zeitung limeandika kuwa: Nchi za Magharibi zimekumbwa na mgawanyiko katika masuala ya kisiasa na uhakika huo umeonekana waziwazi katika mkutano wa viongozi wa nchi 7 zilizopiga hatua kiviwanda wa G7 huko Canada ambao kimsingi ulibadilika na kuwa G6.
Rais Donald Trump wa Marekani siku chache zilizopita aliwaacha bumbuazi viongozi wengine wa G7 katika mkutano wa Canada baada ya kuondoka ghafla katika mkutano huo na kufuta saini yake katika hati ya mwisho ya mkutano huo.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amebainisha masiktiko yake baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kukataa kuidhinisha taarifa ya mwisho ya kikao cha viongozi wa nchi tajiri kiviwanda G7 ambacho kilimalizika juzi huko Quebec, nchini Canada. Merkel amebainisha wazi kuwa nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani.
Naye Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesisitiza kuwa, jibu la Ulaya kuhusu uamuzi huo wa Trump linapaswa kuwa ni mshikamano na ukuruba zaidi katika Umoja wa Ulaya.
Mass ameongeza kuwa uamuzi wa Trump wa kutoafiki taarifa ya mwisho ya kikao cha G7 haukuzishangaza sana nchi shiriki kwani Trump amekiuka mapatano mengine muhimu ya utunzaji mazingira na mapatano ya nyuklia ya Iran.
Baada ya mkutano wa viongozi wa kundi la G7, kumedhihirika hitilafu kubwa na za wazi baina ya Rais Trump na viongozi wa Canada, Ufaransa na Ujerumani. Trump aliondoka mapema kabla ya kikao hicho kumalizika kama ishara ya kubainisha kuchukizwa kwake na tamko la Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na kusema hataunga mkono taarifa ya mwisho ya kikao hicho. Uamuzi huo wa Trump umetajwa kuwa ni pigo kubwa kwa kundi la G7 ambalo linajumuisha Marekani, Canada, Ujerumani, Uingereza,Ufaransa, Italia na Japan.
Hatua hiyo ya Trump itatoa pigo kubwa kwa ushirikiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki na pia ni pigo kubwa kwa uhusiano wa kistratijia wa Canadan na Marekani. Kwa hatua yake hiyo, Trump analenga kung'oa mizizi ya uhusiano na mshikamano wa miongo kadhaa wa kiuchumi, kibiashara, na kiusalama baina ya Marekani na Ulaya. Wakuu wa Ulaya wanajaribu kuzuia hali ya mambo kuwa mbaya zaidi na wanasema hatua ya Trump kutosaini taarifa ya mwisho haimaanishi kila kitu kimekwisha. Kuhusiana na hili, Angela Merkel amesema: "Hatua ya Trump kutangaza kuwa hatatia saini taarifa ya mwisho ya G7 kupitia Twitter ni jambo la kusikitisha. Ameongeza kuwa, 'kikao cha viongozi wa G7 huko Canada hakikuwa mwisho wa ushirikiano wa Ulaya na Marekani lakini akaongeza kuwa, nchi za Ulaya hazipaswi kuitegemea tena Marekani na zinapaswa zenyewe zijiamulie hatima yao.'
Ingawa suala la Marekani kujiondoa G7 halijapewa uzito mkubwa lakini kwa kuzingatia utendaji kazi wa Trump katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa urais wake, nchi zingine sita za kundi la G7 hazitashangaa iwapo Trump ataendeleza mwenendo wake huo wa kupuuza na kubatilisha mikataba ya kimataifa, na hivyo aamue kujiondoa katika kundi hilo. Kwa hivyo nchi hizo sita zinajitayarisha kwa hali kama hiyo.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasema hivi kuhusu suala hilo:"Pengine Trump hajali iwapo atatengwa lakini hata tukibadilika na kuwa kundi la G6 bado tutakuwa nguvu kubwa. Iwapo Trump ataamua kuiondoa Marekani katika nafasi yake duniani, jambo hilo litakuwa na matokeo hasi kwa uchumi na hadhi ya Marekani duniani. Trump anafahamu hili."
Mtazamo wa Trump kuhusu masuala ambayo yamepelekea kuibuka hitilafu baina ya Marekani na Ulaya ni jimbo linaloonyesha kuwa hana nia ya kulegeza msimamo wake bali hata ametoa vitisho kwa kwa nchi za Ulaya na Canada hasa katika masuala ya kibiashara. Trump ameongeza kwa kiwango kikubwa ushuru wa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Ulaya, Canada na Mexico hasa bidhaa za chuma.
Hatua hizo za Trump zimepelekea kuongezeka hitilafu kubwa baina ya Marekani na nchi hizo na kuwepo hatari ya kuibuka vita vya kibiashara kati ya Marekani na nchi hizo. Hali kadhalika nchi za Ulaya pia zimekasirishwa na hatua ya Trump ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA na mapatano mengine muhimu ya mazingira maarufu kama Mapatano ya Tabianchi ya Paris.
Kwa mtazamo wa nchi muhimu katika Umoja wa Ulaya, si tu kuwa sera za Trump zitaidhuru dunia bali zitapelekea kutengwa zaidi Marekani katika uga wa kimataifa.