Friday, December 30, 2016

MAMIA YA MATAKFIRI WANAOREJEA TUNISIA WAKAMATWA

Msemaji wa serikali ya Tunisia ametangaza habari ya kukamatwa mamia ya matakfiri wanaorejea nchini humo kutoka eneo la Mashariki ya Kati.
Iyad Dahmani, msemaji wa serikali hiyo amesema kuwa tokea mwaka 2007 hadi sasa matakfiri wapatao 800 wa Kitunisia wametiwa mbaroni na kufungwa jela baada ya kurejea nchini humo kutokea Syria, Iraq na Libya na kwamba hivi sasa wako chini ya uangalizi mkali. Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Youssef Chahed, Waziri Mkuu wa Tunisia amesema kuwa serikali yake haijatia saini mkataba wowote wa kurejeshwa nchini humo magaidi wa kitakfiri na kwamba  serikali hiyo haiungi mkono kurejea nchini humo kwa magaidi hao.
Youssef Chahed, Waziri Mkuu wa Tunisia
Wiki iliyopita, Hadi Majdub, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia alitangaza habari ya kurejkea nchini matakfiri 800 na kuongeza kuwa viongozi wa nchi hiyo wana habari kamili kuhusiana na magaidi hao. Tokea kuanza kwa vita huko Syria maelfu ya Watunisia waliamua kujiunga na kundi la kigaidi la Daesh na kushiriki katika vitendo vya kinyama na kigaidi dhidi ya wananchi wa Syria. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni ambapo kundi hilo limekuwa likidhoofika siku baada ya siku kufuatia kushindwa katika medani za vita katika nchi hiyo na Iraq, wanachama wa Daesh wamekuwa wakitafuta njia za kurudi katika nchi zao, jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa nchi hizo na hasa wa Tunisia.

BURUNDI YATISHIA KUISHTAKI AU NA KUONDOA ASKARI WAKE SOMALIA

Burundi imetishia kuushataki Umoja wa Afrika AU sambamba na kuwaondoa askari wake nchini Somalia wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Amisom.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesema askari wa nchi hiyo wanaohudumu katika kikosi cha Amisom hawajalipwa mishahara na marupurupu yao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na ndiposa serikali yake inataka kuwaondoa nchini Somalia, mbali na kuishtaki AU.
Amesema iwapo kadhia hiyo ya mshahara haitakua imepatiwa ufumbuzi kufikia mwezi ujao, serikali yake haitakuwa na chaguo jingine ghairi ya kuwaondoa askari wa nchi hiyo Somalia.
Burundi ambayo ina askari 5,432 ndani ya Amisom, ni nchi ya pili baada ya Uganda kwa kuwa na idadi kubwa ya askari wa kulinda amani nchini Somalia.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais wa Burundi amesema nchi hiyo itaushtaki Umoja wa Afrika kwa kukiuka muafaka uliofikiwa na pande zote kuhusiana na mishahara ya askari wa Amisom.
Amisom ilijikuta katika kipindi kigumu cha kuwalipa mishahara wanajeshi zaidi ya 22 elfu wa nchi za Afrika zilizotuma askari wake Somalia zikiwa ni pamoja na Kenya, Ethiopia na Djibouti, baada ya Umoja wa Ulaya EU kupunguza bajeti yake kwa kikosi hicho cha kulinda amani, kwa asilimia 20 mapema mwaka huu.
Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabaab likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata wa nchi jirani. 

NAIBU KATIBU MKUU WA UN AHIMIZA UMOJA NA MSHIKAMANO WA WALIMWENGU

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa nchi zote duniani kuimarisha umoja na mshikamano na kujiepusha na hitilafu na mifarakano.
Jan Eliasson mbaye muda wake wa kuhudumu katika cheo hicho unamalizika kesho sambamba na kumalizika mwaka huu wa 2016 amesema umoja na mshikamano ndiyo haja kubwa zaidi ya dunia ya sasa na kuongeza kuwa, kuna haja ya kutafakari na kutafuta njia ya kutatua migogoro ya dunia kama suala la wahamiaji, wakimbizi na kusitishwa vita katika maeneo mbalimbali.
 
Jan Eliasson
Eliasson pia amewataka viongozi wa nchi mbalimbali kuacha tabia ya kusisitiza juu ya migawanyiko ya kiutaifa, kikabila au kidini. Adha amesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa haki za binadamu.
Kuhusu suala lililomkatisha tamaa zaidi kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson  amesema ni maafa ya Syria na kwamba Umoja wa Mataifa umeshindwa kukomesha mgogoro huo.
Wasyria wakigangaika kutafuta makimbilio
Amesema mgogoro wa Syria umesasababisha mauaji ya mamia ya maelfu ya binadamu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi katika nchi nyingine. Amesisitiza kuwa mgogoro wa Syria umesababisha ukosefu wa uthabiti katika siasa za kimataifa.

NDEGE YA UTURUKI YAWAHAMISHIA YEMEN MAGAIDI WA ISIS KUTOKA ALEPPO

Duru za Yemen zimeripoti kuwa, ndege moja ya Uturuki imewahamishia nchini humo makumi ya magaidi wa Daesh (ISIS) kwa kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden, kusini mwa Yemen, baada ya magaidi hao kufurushwa nchini Syria.
Mtandao wa habari wa al Masirah wa Yemen umeripoti kuwa, ndege ya Uturuki iliyokuwa na magaidi 150 waliofurushwa katika mji wa Halab (Aleppo) wa kaskazini magharibi mwa Syria, imetua katika uwanja huo, ikiwa ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Yemen. Tarehe 22 Disemba mwaka huu, jeshi la Syria lilitangaza kukombolewa kikamilifu mji wa Halab baada ya magaidi wote kuukimbia mji huo baada ya kuukalia kwa zaidi ya miaka minne.
Duru za usalama za Yemen zimetangaza kuwa, ndege ya Uturuki iliyowabeba magaidi hao iliongozwa na vikosi vamizi ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambavyo vinashiriki katika mashambulizi ya kivamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen.

Vile vile mtandao wa habari wa al Masirah umesema kuwa, ndege hiyo ya Uturuki itabeba mamluki 158 wa Saudi Arabia waliojeruhiwa na wanajeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen katika mkoa wa Ta'izz. Majeruhi hao watatibiwa katika hospitali za Uturuki. Uturuki inatajwa kuwa moja ya waungaji mkono wakuu wa magenge ya kigaidi nchini Syria kama ambavyo pia inalaumiwa kwa kutoa mafunzo kwa magenge ya kigaidi yanayofanya jinai ndani ya Syria.
Hadi sasa mashambulizi ya kivamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen yameshaua watu zaidi ya 11,400, kwa mujibu wa kundi la haki za binadamu lisilo la kiserikali la Yemen lijulikanalo kwa jina la Kituo cha Kisheria kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Maendeleo

ISRAEL YAZIDISHA HARAKATI ZA KUIYAHUDISHA QUDS TUKUFU

Duru za Palestina zimetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umechimba mashimo mapya chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Habari hiyo imetangazwa na Kamati ya Kiislamu na Kikristo kwa Ajili ya Kulinda Quds na Matukufu yake. Katibu Mkuu wa kamati hiyo Dk, Hanna Issa ametahadharisha juu ya hatari ya mashimo hayo ya chini ya ardhi kwa majengo na taasisi za Msikiti wa Al-Aqsa na kueleza kwamba, idadi ya mashimo hayo ya chini kwa chini katika mji wa Quds ambayo yanaviunganisha pamoja vitongoji wa walowezi wa Kizayuni yamefikia 27.

Image Caption
Tangu utawala wa Kizayuni wa Israeli ulipouvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji wa Quds mwaka 1967 hadi sasa unaendelea kuchimba mashimo ya chini ya ardhi katika mji huo hasa katika eneo lake la kale na kandokando mwa Msikiti wa Al-Aqsa ili kuwalazimisha Wapalestina wayahame maeneo hayo na kuweza kuyadhibiti maeneo yanayozunguka msikiti huo. Ili kuharakisha zoezi la kufikiwa lengo hilo na kuvunja Msikiti wa al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, utawala huo ghasibu umekuwa ukichimba mashimo chini ya eneo hilo takatifu na kandokando yake kwa shabaha ya kudhoofisha msingi na nguzo zake. Suala hilo linahatarisha na kuzidisha uwezekano wa msikiti huo kuporomoka na kuvunjika iwapo kutatokea tetemeko dogo la ardhi na matukio mengine kama hayo. Vilevile Israel inafanya mikakati ya kuanzisha tetemeko la makusudi la ardhi kwa kulipua maeneo ya chini ya Msikiti wa al Aqsa, ili ionekane kwamba, uharibifu wa msikiti huo umetokana na suala la kimaumbile. Kwa sababu hiyo duru za kuaminika zinasema, njama na mipango ya utawala haramu wa Israel ya kuvunja Msikiti wa al Aqsa imeingia katika awamu nyeti na hatari sana.

Msikiti wa al Aqsa
Kwa miaka mingi sasa Israel imekuwa ikitekeleza mpango wa kubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Quds tukufu kwa kuharibu turathi za Kiislamu na za kale za mji huo na kuweka badala yake alama za Kiyahudi. Katika mkondo huo Israel imekuwa ikiharibu misikiti, majumba ya kihistoria, maeneo ya makaburi ya kale, vituo vya kiutamaduni, mashamba na nyumba za Wapalestina na kujenga maabadi za Wayahudi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Hayo yanafanyika licha ya kwamba maazimio nambari 242 na 338 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vilevile kifungu nambari nne cha Mkataba wa Geneva vimepiga marufuku aina yoyote ya ujenzi na kubadilisha utambulisho wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.  

Mashimo yanayochimbwa na Israel chini ya Msikiti wa al Aqsa
Jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kama zile za kuharibu au kuvunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu au kuvamia maeneo hayo na kuwafukuza Wapalestina ni kielelezo cha siasa za kibaguzi za utawala huo dhidi ya wafuasi wa dini za mbinguni na uhuru wa kuabudu. Kwa msingi huo kuna udharura kwa jumuiya za kimataifa kuchukua msimamo mmoja na madhubuti wa kukabiliana kivitendo na siasa hizo za kibaguzi za Israel na zisitosheke kutoa maazimio yasiyokuwa na dhamana ya utekelezaji dhidi ya utawala huo.

NKURUNZINZA: HUENDA NIKAGOMBEA TENA URAIS 2020

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi amesema kuwa, huenda akagombea tena urais kwa kipindi cha nne mfululizo kama wananchi wa Burundi watamtaka kufanya hivyo.
Nkurunziza ambaye uamuzi wake wa kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo umeitumbukiza Burundi kwenye mgogoro mkubwa amesema katika mkutano mmoja uliofanyika mjini Rutuna, kusini mashariki mwa Burundi kwamba: "Kwa vile tunaheshimu utawala wa sheria na iwapo wananchi watapitisha kuwa, kugombea tena si kuvunja sheria, na kama wananchi wataomba jambo hilo, hatuwezi kusaliti imani  ya nchi, hatuwezi kusaliti imani ya wananchi.
Aidha amesema, kuna uwezekano katiba ya Burundi ikafanyiwa marekebisho na kuondoa kipengee cha ukomo wa kugombea urais nchini humo na pia kipindi cha miaka mitano uongozini.

Askari wa Burundi wanatuhumiwa kuwanyanyasa vibaya raia

Wakati aliposhiriki kwenye uchaguzi kwa mara ya tatu mfulilizo mwaka 2015, Nkurunziza alidai kuwa kuchaguliwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kulikuwa kwa kipindi cha mpito baada ya vita vya ndani hivyo alikuwa na haki ya kugombea urais kwa mara ya tatu.
Hata hivyo wapinzani waliilalamikia vikali hatua hiyo na kusema kuwa ni kinyume na makubaliano ya Arusha Tanzania yanayompa haki mtu kuongoza Burundi kwa vipindi viwili.
Maelfu ya wananchi wamekuwa wakimbizi, tangu Rais Nkurunziza alipoamua kugombea urais kwa kipindi cha tatu mfululizo

Tangu wakati huo hadi hivi sasa Burundi imeshuhudia machafuko mengi, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakiripoti kutokea kesi chungu za uvunjaji wa haki za binadamu, mateso, udhalilishaji wa kijinsia, kutiwa mbaroni watu kwa umati na kupotezwa bila kujulikana waliko.
Burundi ina historia ndefu ya machafuko baina ya makabila ya Kihutu na Kitutsi yaliyopelekea nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika kushuhudi miaka 12 ya mapigano ya ndani yaliyoanza mwaka 1993 na kumalizika 2006 kwa mujibu wa Makubaliano ya Arusha. 

MAABARA YA KISASA YAZINDULIWA MASHARIKI YA KATI NA SHIRIKA LA NDEGE LA ETIHAD


SHIRIKA la Ndege la Etihad kupitia Kitengo chake cha Uhandisi (Etihad Airways Engineering) kwa kushirikiana na Lental Textiles AG wamezindua maabara ya kipekee ya kwanza Mashariki ya Kati kwa ajili ya wateja wa kanda hiyo walio sekta ya anga na waendeshaji mashirika ya uzalishaji na ubunifu.Maabara hiyo ambayo ipo ndani ya kituo cha uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad karibu kabisa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abu Dhabi itakuwa inatoa huduma mbalimbali ikiwemo vipimo vya kuwaka kwa moto, joto, moshi n.k.
Aidha, maabara hiyo itaenda sambamba na hadhi ya ubora wa Kimataifa ISO 17025 na vipimo vyote vitafanyika kwa mujibu wa Kanuni za Anga za imataifa FAR/CS25.853.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad Jeff Wilkinson alisema, “Tunatoa huduma zilizotukuka kwenye matengenezo ya ndege na ufumbuzi wa kiuhandisi katika soko la anga duniani na kwa ajili ya aina zote za ndege za kibiashara.
“Kupitia ushirikiano wetu huu na Lantal, itakuwa rahisi sasa na haraka kwa kwa wateja wa sekta ya anga katika Ukanda kupata huduma bora za vipimo katika kituo chetu cha Abu Dhabi,” alisema.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Lantal, Dkt. Urs Rickenbacher alisema, “Maabara yetu ya Lantal kwa ajili ya vipimo nchini Uswisi inajulikana vema kwa huduma zake bora na haraka. Kwa sasa tunalo soko kubwa barani Ulaya na sasa maabara yetu hapa Abu Dhabi tukishirikiana na Kitengo cha Uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad (Etihad Aiways Engineering) litatuwezesha kutoa huduma kwa ukaribu zaidi na wateja wetu wa Mashariki ya Kati,”.

DRC WAPINZANI WASEMA MAZUNGUMZO YALEGALEGA

Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanasema mazungumzo ya namna Rais Joseph Kabila atakavyoondoka madarakani yanalegalega na yamkini yakasambaratika.
Kwa mujibu wa FĂ©lix Tshisekedi mmoja kati ya vinara wa upinzani, pande husika katika mazungumzo hayo zinakaribia kusambaratika kuliko kupata suluhisho.
Leo mazungumzo baina ya serikali na vyama vya upinzani chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki yamefanyika mjini Kinshasa. Jana Alhamisi makasisi wapatanishi walikutana na Rais Kabila pamoja na kiongozi mkongwe wa upinzani Etienne Tshisekedi ili kujaribu kufikia mwafaka.
Kwa mujibu wa mapatano yaliyopendekezwa, Kabila hatabadilisha katiba ili ashiriki katika uchaguzi mkuu mwakani. Aidha utawala wake wa mihula miwili ambao ulimalizika Disemba 19 utaongezwa hadi mwaka 2018.
Etienne Tshisekedi
Mazungumzo baina ya pande mbili yalikaribia kumalizika wiki jana ili kuandaa mazingira ya ukabidhianaji madaraka kwa amani kupitia mchakato wa demokrasia kwa mara ya kwanza tokea nchi hiyo ijinyakulie huru mwaka 1960. Hata hivyo kizingiti kikuu kimeripotiwa kuwa ni iwapo waziri mkuu atoke mrengo mkuu wa upinzani. Aidha kumekuwepo mvutano kuhusu Tume ya Uchaguzi ambayo wapinzani wanasema inaegemea upande wa serikali.
Watu 40 walipoteza maisha wiki jana mjini Kinshasa katika maandamano ya kutaka Kabila aondoke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo tokea mwaka 2001 wakati baba yake, Laurent Desire Kabila, alipouawa.

SERIKALI YA MISRI YAPITISHA MPANGO WA KUIPATIA SAUDIA VISIWA

Ripoti kutoka Misri zinaeleza kuwa licha ya malalamiko ya wananchi na upinzani wa mahakama, serikali ya nchi hiyo imepitisha mpango wa kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir. Duru za habari za Misri zimetangaza kuwa serikali imeidhinisha mpango huo na tayari imeshaupeleka bungeni.
Kwa mujibu wa duru hizo, Mahakama Kuu ya Misri imepinga mpango huo na inatazamiwa kutoa hukumu yake rasmi juu ya suala hilo katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Baadhi ya shakhsia na wataalamu wa sharia nchini Misri wanaitakidi kuwa uamuzi wa kupitishwa mpango wa kuipatia Saudia visiwa viwili ambavyo Wamisri waliowengi wanaamini ni milki ya nchi yao una uhusiano na kadhia ya kamati za sharia za bunge la Misri.
Ahmad Suleiman, waziri wa zamani wa sharia ameashiria suala hilo na kueleza kwamba lengo la mpango huo ni kukabiliana na mahakimu wanaotoa hukumu kinyume na matakwa ya viongozi wa serikali na badala yake kuzingatia maslahi ya taifa tu. Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuwaondoa mahakimu wanaotoa hukumu zisizoendana na mitazamo ya serikali.
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri (kulia) na Mfalme Salman wa Saudi Arabia
Mapema mwaka huu, serikali ya Misri ilitiliana saini mkataba wa mipaka ya bahari na Saudia na kutangaza kufuatia hatua hiyo kwamba visiwa vya Tiran na Sanafir viko kwenye maji ya ardhi ya Saudia.
Imeelezwa kuwa serikali ya Cairo itapatiwa dola bilioni 20 na Saudi Arabia kwa kuupatia utawala wa kifalme wa Aal Saud visiwa hivyo.
Uamuzi huo umelaaniwa na kulalamikiwa vikali na wananchi, duru za kisiasa, vyombo vya habari na asasi za kiraia nchini Misri ambao wamemtuhumu Rais Abdel Fattah el Sisi kuwa amefanya uhaini na kuziuza ardhi za nchi hiyo.
Hata hivyo katika jibu alilotoa kuhusiana na tuhuma hizo El Sisi amesema hajaipatia Saudia hata chembe ya ardhi ya Misri bali ameirejeshea nchi hiyo haki yake…/