Friday, March 30, 2018

POLISI TANZANIA: HATUJABAINI SILAHA ILIYOTUMIKA KUMUUA AKWILIN, LEMA ASHANGAA

Polisi Tanzania:  Hatujabaini silaha iliyotumika kumuua Akwilina, Lema ashangaa
Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania, Lazaro Mambosasa, amesema kuwa hadi sasa bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa kupigwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Hata hivyo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameshangazwa na taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kuhusu kutojulikana silaha iliyotumika kumuua Akwilina na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Nimeitafakari kauli ya Mambosasa inayohusu tukio la Akwilini kuhusu silaha iliyotumika, bila shaka kuna dhambi kubwa inapangwa nawasihi Wana CHADEMA kuwa makini wakati huu kwani si ajabu ukasikia kuwa Ile silaha iliyotumika kumuua Akwilini imekutwa nyumbani kwa Kiongozi wa CHADEMA” -Lema

Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alisema jana Ijumaa mbele ya waandishi wa habari bado hawajabaini ni silaha gani ilitumika katika tukio la mauaji ya Akwilina Akwini, ambaye kifo chake kimezusha malalamiko makubwa ya asasi mbalimbali na kiraia nchini Tanzania.
Akwilina Akwilini, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
“Bado tunaendelea na upelelezi wa tukio hili. Hatujajua ile silaha iliyotumika hadi kumpata Akwilina kwa sababu askari walikuwa wengi siku ile na hakukuwa na ushahidi ni yupi aliyetenda kosa hilo.“ Amesema Mambosasa. Hii ni katika hali ambayo, tarehe 18 Februari mwaka huu Kamanda Lazaro Mambosasa alinukuliwa akisema kuwa, jeshi la polisi linawashikilia askari wake sita na silaha zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Polisi wakituliza ghasia nchini Tanzania
Akwilina Akwilini, aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe 16 Februari mwaka huu, wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) waliokuwa wanaamdamana kuelekea ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kushinikiza mawakala wao kupatiwa barua za viapo vyao kwa ajili ya kusimamia uchaguzi mdogo uliopita wa jimbo hilo.

AL SISI ATANGAZWA MSHINDI WA KITI CHA URAIS WA MISRI

Al Sisi atangazwa mshindi wa kiti cha Rais wa Misri
Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ametangazwa mshindi wa uchaguzi tata wa rais uliofanyika Jumatatu iliyopita, kwa kuzoa asilimia 92 ya kura zote zilizopigwa.
Uchaguzi wa Rais wa Misri uliofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 26 Machi, ulimalizika juzi tarehe 28. Katika uchaguzi huo al Sisi alichuana na Moussa Mostafa Moussa wa chama cha al Ghad ambaye ametajwa na vyombo vya habari kuwa hakuwa mpinzani wa al Sisi bali alichomekwa kwenye kinyang'anyiro hicho kuhalalisha zoezi hilo.
Mambo mawili yametajwa kuwa sababu kuu za ushindi wa Abdul Fattah al Sisi hata kabla ya uchaguzi huo kufanyika.
Kwanza ni kukandamizwa kambi kuu ya upinzani katika kipindi chote cha uongozi wa miaka minne iliyopita ya utawala wa al Sisi. Kijadi, mpinzani mkuu wa kiongozi wa sasa wa Misri alipaswa kuwa mgombea yeyote wa harakati ya Ikhwanul Muslimin. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita watawala wa Misri wamefanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, harakati hiyo inakandamizwa, viongozi wake wanaoswekwa jela na wafuasi wao wanahukumiwa vifungo au hata adhabu ya kifo. Baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak katika mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011, harakati hiyo ilipata anga ya pumua kidogo na mgombea wake akashinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika nchini humo. Hata hivyo serikali ya Muhammad Mursi haikuishi zaidi ya mwaka mmoja. Serikali hiyo ya kwanza kuchaguliwa na wananchi kwa njia za kidemokrasia, iliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdul Fattah al Sisi. 
Sami Hafez Anan
Sababu kuu ya pili ya ushindi wa al Sisi ni kubinywa na hata kukamatwa wapinzani mashuhuri wa kiongozi huyo kabla kidogo ya zoezi la uchabuzi wa rais. Serikali ya Cairo iliwazuia wagombea mashuhuri kama Ahmad Shafiq, Sami Hafez Anan, Abdel Munim Abul Futuh kujitosa katika kinyang'anyiro hicho kwa kutumia visingizio mbalimbali. Hata Moussa Mustafa Moussa aliyechuana na al Sisi katika uchaguzi huo anajulikana kuwa muungaji mkono wa Abdul Fattah al Sisi.
Uchaguzi wa rais uliofanyika Misri ulifanyika kwa kuwa hakukuwa na budi kufanyika, na al Sisi alilazimika kuitisha zoezi hilo. Mchambuzi wa masuala ya siasa Hassan Shukri anasema: Uchaguzi wa rais uliofanyika Misri haukuwa ushindani baina ya wagombea wawili bali lilikuwa zoezi la kuhalalisha utawala wa al Sisi. Hata hivyo siasa za ngumi ya chuma zinazotekelezwa na al Sisi akisaidiwa na jeshi tangu miaka minne iliyopita, kutotimizwa ahadi zilizotolewa na kiongozi huyo kwa wananchi na kupuuzwa au kukanyagwa demokrasia na uhuru vimeshusha chini zaidi imani ya Wamisri kwa kiongozi huyo." 
Jenerali Abdul Fattah al Sisi
Ni kwa kutilia maanani sababu hizo mbili ndiyo maana Abdul Fattah al Sisi akaingia kwenye klabu ya viongozi wa nchi za Kiarabu wanaoshinda chaguzi za rais kwa kupata eti asimia zaidi ya 90 ya kura zilizopigwa! Pamoja na hayo wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii wanatarajia kuwa, jenerali huyo mstaafu hatafanya marekebisho ya katiba yanatakayomruhusu kubakia madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa vipindi viwili kama wafanyavyo baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika na Kiarabu.

TUNDU LISSU : KINACHOWAPATA VIONGOZI WA UPINZANI TANZANIA, NI NJIA YA KUELEKEA IKULU

  
Tundu Lissu: Kinachowapata viongozi wa upinzani Tanzania, ni njia ya kuelekea Ikulu       
Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema kuwa, kile kinachowapata viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA), ni maandalizi ya upinzani huo kuingia madarakani.
Tundu Lissu ameyasema hayo ikiwa ni baada ya viongozi sita wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti Taifa wa chama Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Vincent Mashinji, Manaibu Katibu Mkuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, kushtakiwa kwa makosa manane na kisha kunyimwa dhamana.
Viongozi wa Chadema wakiwa kwenye gari la polisi baada ya kutiwa mbaroni
Kadhalika Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu, amefafanua kuwa, kilichowapata viongozi hao wa upinzani nchini Tanzania hakiwezi kuzima taa ya madai kwa ajili ya demokrasia ya kweli nchini humo. Viongozi hao wa chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA), walipelekwa jela siku ya Jumanne baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka manane yakiwamo ya kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline, uasi, kuhamasisha chuki kati ya wanajamii na kuchochea ghasia nchini Tanzania.
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania
Hayo yanajiri katika hali ambayo siku chache zilizopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliviambia vyombo vya habari kwa kuzituhumu asasi za serikali ya Dar es Salaam ikiwemo polisi kwamba, zilikuwa zinapanga mkakati wa kuwafungulia kesi ya mauaji na uhaini baadhi ya viongozi wa chama chake. Kwa mujibu wa Mbowe, lengo la kutekelezwa mkakati huo ni kuhakikisha kuwa viongozi hao wanawekwa mahabusu kwa muda mrefu ili kufifisha na kuua kabisa upinzani nchini.

WAPALESTINA 8 WAUAWA SHAHIDI NA JESHI LA ISRAEL KATIKA MAANDAMANO YA SIKU YA ARDHI

Wapalestina 8 wauawa shahidi na jeshi la Israel katika maandamano ya Siku ya Ardhi
Kwa akali Wapalestina wanane wameuawa shahidi na wanajeshi katili wa Israel katika maandamano ya Siku ya Ardhi, ya kulaani hatua ya utawala huo ghasibu ya kupora ardhi zao, yaliyofanyika leo karibu na uzio wa kibaguzi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imesema mbali na Wapalestina wanane kuuawa shahidi kwa kumiminiwa risasi na wanajeshi katili wa Israel, wengine zaidi ya 550 wamejeruhiwa vibaya.
Kituo cha Kutetea Haki za Wapalestina cha Adalah kimelaani vikali mauaji hayo, na kueleza kusikitishwa kwake na kitendo cha jeshi la Israel kutumia risasi hai, vifaru na maroketi dhidi ya waandamanaji ambao hawana ulinzi. 
Kituo hicho kimesema mauaji hayo dhidi ya Wapalestina waliokuwa wakiandamana kutetea ardhi zao zilizoporwa ni kinyume cha sheria za kimataifa.
Siku ya Ardhi huadhimishwa Machi 30 kila mwaka
Maelfu ya Wapalestina wamejitokeza kushiriki maandamano hayo, licha ya idadi kubwa ya wanajeshi wa Israel waliojizatiti kwa silaha nzito kuuzingira uzio huo wa Gaza, na licha ya utawala huo haramu kutumia fatua za Saudi Arabia kuwashawishi Wapalestina hao kutoshiriki maandamano hayo.
Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, maandamano ya kwanza ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kulaani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina.
Waarabu sita wa Israel ambao hawakuwa wamejizatiti kwa silaha waliuawa na askari wa Kizayuni katika maandamano hayo yaliyofanyika Machi 30 mwaka 1976.

UTAFITI: WAKONGOMANI 8 KATI YA 10 HAWAMUUNGI MKONO RAIS KABILA WA DRC

Utafiti: Wakongomani 8 kati ya 10 hawamuungi mkono Rais Kabila wa DRC
Utafiti mpya wa maoni umeonyesha kuwa, kwa kila raia kumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanane hawamungi mkono Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.
Utafiti huo uliofanywa mwezi jana na shirika la utafiti la Congo Research Group CRG likishirikiana na Kituo cha Utafiri wa Maoni cha BERCI katika Chuo Kikuu cha New York unaonyesha wazi kuwa, akthari ya Wakongomani wamechoshwa na uongozi wa miaka 17 wa Rais Kabila na wangetaka kumuona akiachia ngazi.
Joseph Kabila alikataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula wake wa utawala kikatiba mwaka 2016, na mpaka sasa hajajitokeza hadharani kusema iwapo ataachia ngazi baada ya uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu au la.
Moise Katumbi, mwanasiasa mjasiriamali wa DRC
Kwa mujibu wa utafiti huo wa maoni uliowashirikisha Wakongamani elfu moja katika mikoa yote 26 ya nchi hiyo, asilimia 95 ya waliohojiwa wanasema wako tayari kushiriki uchaguzi rais wa mwezi Disemba; ambapo asilimia 26 wanasema wangelimchagua Moise Katumbi, kiongozi wa upinzani aliyeko uhamishoni, huku asilimia 13 wakisema wangelimchagua mwanasiasa mwingine wa upinzani Felix Tshisekedi kurithi mikoba ya Kabila.
Utafiti mwingine wa maoni uliofanywa mwaka mmoja uliopita na CRG na BERCI ulionyesha kuwa, asilimia 38 ya wapiga kura nchini humo wako tayari kumpigia kura Katumbi, na yumkini kiwango hicho kimeshuka ikilinganishwa na utafiti wa mwaka huu, kutokana na mwanasiasa huyo tajiri kutokuweko nchini kwa miaka miwili sasa

Sunday, March 25, 2018

RAIS WA IRAN LEO ANAELEKEA TURKMENISTAN NA JAMUHURI YA AZERBAIJAN

Rais wa Iran leo anaelekea Turkmenistan na Jamhuri ya Azerbaijan
Rais Hassan Rouhani wa Iran leo anaanza safari ya siku mbili ya kuzitembelea nchi jirani za Turkmenistan na Jamhuri ya Azerbaijan kwa lengo la kujadiliana na viongozi wa nchi hizo uhusiano wa pande mbili na matukio ya hivi karibuni ya kieneo.
Akiongoza ujumbe wa ngazi za juu, Rais Rouhani ataelekea Ashgabat, mji mkuu wa Turkmenistan katika duru ya kwanza ya safari yake kufuatia mwaliko wa rais mwenzake wa nchi hiyo Gurbanguly Berdimuhamedow.
Kwa mujibu wa Parviz Ismaili,  mkuu wa kitengo cha habari katika Ofisi ya Rais wa Iran, katika safari hiyo nchi hizo mbili zitatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano hasa katika sekta za biashara. Marais Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan (kushoto) na Rouhani wa Iran katika mkutano wao mjini Tehran mwaka jana
Aidha akiwa Turkmenistan, Rais Rouhani atatembelea mji wa kale wa Merv siku ya Jumatano. Baada ya hapo Rouhani ataelekea Baku, mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan ambapo atafanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Ilham Aliyev. Inatazamiwa pia katika safari hiyo nchi mbili zitatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirkiano wa kiuchumi.

WASI WASI WAMAREKANI KUHUSIANA NA VITA VYA KIBIASHARA KATI YA NCHI YAO NA CHINA

Wasi wasi wa Wamarekani kuhusiana na vita vya kibiashara kati ya nchi yao na China
Suala la Rais Donald Trump wa Marekani kutia saini dikrii ya kupandishwa ushuru wa forodha wa biadhaa za China, limeibua tofauti kubwa za kibiashara kati ya Marekani na China.
Kufuatia hatua hiyo, raia hususan wakulima wa Marekani wamekumbwa na wasi wasi mkubwa juu ya hatua zinazoweza kutekelezwa na China katika uga wa kibiashara. Wasi wasi huo umeibuka baada ya radiamali ya China ya kutangaza kwamba Beijing haitorudi nyuma katika mwenendo huo. Kwa kuzingatia hali mbaya ya uchumi wa Marekani kwa sasa hususan katika sekta ya kilimo, weledi wengi wanaamini kwamba, uzalishali ndio njia pekee inayoweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na hali mbaya.
Marais wa China na Marekani
Hata hivyo kwa kutiwa saini dikrii hiyo na kadhalika hatua mkabala za Wachina katika uwanja huo, kunaifanya njia ya wokovu kufungwa na hivyo kuisababishia matatizo zaidi ya kiuchumi jamii ya Marekani. Kufuatia hali hiyo, Cui Tiankai, balozi wa China mjini Washington sambamba na kuonyesha kutofurahishwa na maamuzi ya serikali ya Marekani kuhusiana na kadhia hiyo amesema kuwa, kamwe China haikupendelea kuingia katika vita vya kibiashara na Marekani, lakini akatahadharisha kwamba, iwapo Beijing italazimika kuingia katika uwanja huo, basi haitorudi tena nyuma. Radiamali hiyo kali ya China, imeisababishia wasi wasi mkubwa jamii ya kiuchumi ya Marekani kiasi cha kuyafanya masoko ya hisa nchini humo kuporomoka.
Mgogoro kati ya Marekani na China
Timu ya Rais Donald Trump wa Marekani inaamini kwamba, kuzidishwa ushuru wa forodha kwa bidhaa za China kwa kiasi fulani kutapelekea kushuka kwa nakisi ya kibiashara ya Marekani ambapo licha ya kuwa huenda suala hilo likawa na madhara kwa sekta tofauti za kiuchumi nchini, lakini kwa muda mrefu litakuwa na maslahi kwa uchumi na jamii nzima ya Marekani. Peter Navarro, mshauri mkuu wa rais katika masuala ya biashara na viwanda, anasema kuwa, kupungua nakisi ya kibiashara, ni jambo linalotishia usalama wa taifa na kuifanya nchi hiyo kutegemea madeni na uwekezaji wa kigeni. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kutekelezwa dikrii hiyo mpya ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa mashirika makubwa kama vile Boeing na Apple, kutakuwa na madhara makubwa sambamba na kupelekea makumi ya maelfu ya watu kupoteza fursa zao za kazi ndani ya nchi hiyo. Kadhalika iwapo China itachukua hatua ya kulipiza kisasi, basi sekta ya kilimo ya Marekani hususan uzalishaji wa mazao ya Soya, nao utaathirika zaidi huku makumi ya maelfu ya watu pia wakipoteza ajira. 
Mvutano ukiendelea
Jim Byrum, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Marekani, anasema: "Hivi sasa tunashuhudia mgogoro mkubwa. Ninachukia hata kutamka neno 'vita vya kibiashara,'  hata hivyo inaonekana kuwa sisi tayari tumesukumwa kuelekea upande huo." Mwisho wa kunukuu. Inaonekana kuwa, vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinakaribia kutokea. Ni wazi kuwa kupungua uzalishaji ni moja ya matokeo ya siasa ambazo zitasababisha kuongezeka kiwango cha watu wasio na ajira nchini Marekani. Kwa hakika wasi wasi wa mashirika na wakulima wa Marekani ni jambo lililo mahala pake, kwani hatua mkabala ya Wachina itazisababishia madhara makubwa sekta tofauti za kiuchumi nchini Marekani.