Sunday, March 25, 2018

SERIKALI YA NIGERIA INAFANYA MAZUNGUMZO NA BOKO HARAMU YA UWEZEKANO WA KUSITISHA MAPIGANO

Serikali ya Nigeria inafanya mazungumzo na Boko Haram ya uwezekano wa kusitisha mapigano
Waziri wa Habari wa Nigeria amesema serikali inafanya mazungumzo na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano, lengo kuu likiwa ni kuhitimisha kikamilifu uadui na uhasama baina ya pande mbili.
Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa kwa serikali ya Abuja kutangaza kuwa inafanya mazungumzo na Boko Haram kuhusu usitishaji mapigano yaliyosababishwa na uasi uliopelekea kuuawa maelfu ya watu tangu mwaka 2009.
"Wengi wakiwa hawajui, kwa muda sasa tumekuwa tukifanya mazungumzo mapana ya kuhitimisha uhasama na waasi" amesema Lai Mohammed, Waziri wa Habari wa Nigeria kupitia taarifa aliyotoa kuzungumzia pia kilichofanyika hadi kupelekea kuachiwa huru zaidi ya wanafunzi wa kike 100 na kundi la kigaidi la Boko Haram wiki iliyopita.
Wasichana hao walitekwa nyara Februari 19 katika mji wa Dapchi kaskazini mashariki mwa Nigeria. Utekaji nyara huo wa wanafunzi wapatao 110 ulikuwa wa idadi kubwa zaidi tangu wanafunzi wa kike wapatao 270 walipotekwa nyara na kundi la kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Chibok ulioko kaskazini mashariki pia mwa Nigeria mwaka 2014.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria akiwa na wanafunzi wa mji wa Dapchi baada ya kuachiwa huru na kuonana nao mjini Abuja
Siku ya Jumatano iliyopita, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliwashangaza wakaazi wa mji wa Dapchi walipoingia na magari mjini humo na kuwaachia huru wasichana hao ambao walisema, wenzao watano walifariki walipokuwa wakishikiliwa na kundi hilo na mmoja mwengine bado hajaachiwa huru.
Kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa Nigeria, makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja kuanzia Machi 19 ndiyo yaliyowezesha Boko Haram kuwaachia huru wasichana hao.../

Thursday, March 22, 2018

KENYA NI MWENYEJI WA WIKI YA KUPAMBANA NA UBAGUZI WA RANGI WA ISRAEL

Kenya ni mwenyeji wa Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel
Duru ya 14 ya 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' inafanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ikijumuisha maonyesho ya filamu, mijadala na matamasha ya kiutamaduni.
Shughuli hiyo ilianza tarehe 12 Machi na itaendelea kwa siku kadhaa zijazo kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) katika utawala haramu wa Israel unaowalenga Wapalestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao.
Filamu kadhaa zinaonyesha kuhusu ubaguzi wa rangi Israel kwa lengo la kuwafahamisha wapenda haki nchini Kenya kuhusu utambulisho wa kibaguzi wa utawala haramu wa Israel. Hafla hizo zimehudhuriwa na watu wa matabaka mbali mbali ya jamii. Mijumuiko ya 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' nchini Kenya imeandaliwa na Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina kwa ushirikiano na Tume ya Haki za Binadamu Kenya, Kituo cha Uadilifu wa Kijamii cha Mathare, Kituo cha Utafiti cha Mau Mau, jumuiya za kijamii za Fahamu, Awaaz na Kituo cha Kulinda na Kutetea Haki kati ya taasisi zinginezo.
Kwa ujumla 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' (Israeli Apartheid Week) hulenga kuwahimiza walimwengu kuunga mkono harakati ya kuusisia kwa kila namna utawala haramu wa Israel. Mwaka huu ''Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel'  ilianza Februari 19 na itaendelea hadi tarehe 17 Aprili' katika miji mbali mbali duniani.

SALAMU ZA PONGEZI ZA TRUMP KWA PUTIN HASIRA ZA WAPINZANI WA RUSSIA NDANI YA UTAWALA WA MAREKANI

Salamu za pongezi za Trump kwa Putin na hasira za wapinzani wa Russia ndani ya utawala wa Marekani
Salamu za pongezi alizotoa rais wa Marekani kwa rais wa Russia kwa ushindi aliopata wa kuchaguliwa tena kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni zimewakasirisha baadhi ya maseneta nchini Marekani.
Seneta wa chama cha Republican John MacCain amemtuhumu Rais Vladmir Putin wa Russia kuwa ni dikteta na kusema kwamba: kwa kumpa salamu za pongezi Vladmir Putin,Trump amewatusi wananchi wote wa Russia ambao wamenyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi huru na wa haki ili kuamua kuhusu mustakabali wa nchi yao, ikiwemo idadi kubwa ya wazalendo wa Russia; watu ambao wamehimili hatari nyingi ili kuweza kutumia haki yao ya kulalamika na kupambana na utawala wa Putin.
Seneta John McCain (kulia) na Rais Vladmir Putin wa Russia
Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo katika uchaguzi wa rais wa Russia uliofanyika hivi karibuni vyama na mirengo tofauti ya kisiasa ikiwemo ya wapinzani wakubwa wa Kremlin ilishiriki kwenye uchaguzi huo kuchuana na rais Putin. Hata hivyo kiongozi huyo ameweza kuvutia kura na mapenzi ya aghalabu ya Warussia kutokana na utendajikazi wake wa miaka 17 hususan mafanikio aliyopata ya kuitatua migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama iliyotokana na kuvunjika Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani na kufufua tena nguvu na satua ya nchi hiyo katika uga wa kimataifa. Hali hiyo imetafsiriwa na kuelezewa na mirengo inayoipinga Russia katika nchi za Magharibi na hasa Marekani kuwa ni udikteta na hila za kutaka kuyatia mkono matokeo ya uchaguzi wa rais wa Russia uliofanyika hivi karibuni. Mrengo huo unaitumia kila fursa ikiwemo ya utoaji salamu za pongezi rais wa Marekani kwa rais wa Russia ili kuvuruga uhusiano wa Washington na Moscow, ilhali kuwasiliana kwa njia ya simu marais wa nchi mbili na kupongezana kwa kushinda katika uchaguzi ni jambo la kawaida na lililozoeleka. Takribani mwaka mmoja na nusu uliopita Putin alimtumia salamu za pongezi Trump aliposhinda uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika mwaka 2016; na hivi sasa baada ya kupita siku mbili tangu kufanyika uchaguzi wa rais wa Russia, Trump naye amefanya vivyo hivyo kupitia mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Vladmir Putin. Lakini yeye amekwenda hata mbali zaidi kwa kueleza matumaini aliyonayo ya kupatikana fursa haraka iwezekanavyo ya kukutana na kufanya mazungumzo na rais wa Russia.
Trump (kulia) na Putin wameshakutana zaidi ya mara moja kwa mazungumzo
Mrengo unaoipinga Russia nchini Marekani una hofu baada ya kuona kwamba, licha ya propaganda kali za kueneza sumu dhidi ya Kremlin kwa kutumia visingizio mbalimbali kama kuingilia Russia uchaguzi wa rais wa Marekani sambamba na tuhuma mpya dhidi ya Moscow za kumpa sumu jasusi wa pande mbili wa Uingereza, Trump angali anafanya kila njia ili kuona uhusiano wa nchi yake na Russia unaboreka.
Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais mwaka 2016 hadi sasa, rais wa sasa wa Marekani amesisitiza mara kadhaa kwamba bila ya kushirikiana na Russia baadhi ya mizozo mikubwa ya kimataifa hususan mgogoro wa vita vya Syria hautoweza kutatuka. Ni kwa sababu hiyo Trump angali anashikilia msimamo wake wa kuendelea kuwa na mawasiliano binafsi na rais wa Russia, kitendo ambacho kwa mtazamo wa baadhi ya watu kama John McCain, mkuu wa kamati ya huduma za vikosi vya ulinzi vya Marekani katika Seneti ya nchi hiyo, ni dhambi isiyosameheka.

Monday, March 5, 2018

MFUASI WA MUGABE AUNDA CHAMA KIPYA CHA SIASA ZIMBABWE KUCHUANA RAIS MNANGAGWA KATIKA UCHAGUZI

Mfuasi wa Mugabe aunda chama kipya cha siasa Zimbabwe kuchuana na rais Mnangagwa katika uchaguzi
Ambrose Mutinhiri, jenerali mstaafu wa jeshi la Zimbabwe na mfuasi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe ameunda chama kipya cha siasa kinachojulikana kama Harakati Mpya ya Kizalendo (NFP) kuchuana na rais Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Mutinhiri, ambaye ni veterani wa vita vya uhuru wa Zimbabwe katika miaka ya 1970 alijitoa kwenye chama tawala cha ZANU-PF na kujiuzulu kiti chake cha ubunge siku ya Ijumaa iliyopita na kukutana na Mugabe siku ya Jumapili kumtaarifu juu ya kinachoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotoa hapo jana, NFP imetangaza kuwa  chama hicho kimeundwa na wananchama wa ZANU-PF na Wazimbabwe waliokasirishwa na utaratibu usio wa kikatiba na wa udhalilishaji uliotumika kumuondoa kihalifu uongozini rais Mugabe na wale kiliowataja kama wahalifu halisi walioiharibu bila ya aibu demokrasia inayochipua ya Zimbabwe.
Rais Emmerson Mnangagwa (kushoto) na Robert Mugabe (kulia)
Hayo yanajiri katika hali ambayo duru za karibu na rais wa zamani wa Zimbabwe zimeripoti kuwa Mugabe ana uchungu wa kuondolewa kwenye kiti cha urais alichokalia kwa miaka 37 na kwamba ametangaza uungaji mkono wake kwa chama kipya cha New Patriotic Front (NFP).
Mnamo mwezi Januari mwaka huu rais Emmerson Mnangagwa alitangaza kuwa uchaguzi ujao wa Rais, Bunge na serikali za mitaa nchini Zimbabwe utafanyika katika mazingira huru na ya haki.../

KUONGEZEKA BAJETI YA KIJESHI YA CHINA KATIKA MWAKA 2018

Kuongezeka bajeti ya kijeshi ya China katika mwaka 2018
Serikali ya China imetangaza kuongeza bajeti yake ya kijeshi katika mwaka huu wa 2018.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bajeti ya kijeshi ya China katika mwaka huu wa 2018 itaongezea kwa asilimia 8.10. Bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo imetangazwa kuwa  dola  bilioni 175. Duru za kijeshi nchini China zinasema kuwa bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo bado ni ndogo ikilinganishwa na bajeti ya Marekani ya dola bilioni 700. Pamoja na hayo, hatua ya China ya kuongeza bajeti yake ya kijeshi inahesabiwa kuwa ni aina fulani ya radiamali ya nchi hiyo kwa mipango ya kijeshi ya kichokozi ya Marekani katika eneo la mashariki mwa Asia; ambayo imeshika kasi katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa hivi karibuni wa utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Rais Donald Trump wa Marekani 
Katika stratejia yake mpya ya usalama wa taifa iliyoitangazwa hivi karibuni, Marekani inahisi kuwa China  ni nchi tishio zaidi dhidi yake na inasisitiza kuhitimishwa nguvu hiyo ya China. Moja ya siasa za kistratejia za Marekani mkabala na China ni kuona kunafanyika jitihada za kuishawishi Beijing izidishe bajeti yake ya kijeshi sambamba na kuiingiza katika mashindano ya kijeshi kati yake na Marekani na waitifaki wake katika eneo kama vile Japan na Korea ya Kusini. Siasa ambazo zinatajwa na viongozi wa China kuwa ni siasa za fikra za vita baridi za Washington; na kuamini kuwa Marekani inafanya kila iwezalo ili kuifanya China kuwa na mustakbali kama ule wa Umoja wa Kisovieti. Ndio maana China haipendelei kuingia katika mashindano ya kijeshi na Marekani licha  ya kuzidisha bajeti yake ya kijeshi. 
Nikita Danuk Naibu Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kistratejia ya Russia anasema kuwa: Rais Donald Trump hataki kuharibu misingi ya  ushirikiano kati ya Washington na Beijing. Amejikita zaidi na kuzingatia kubadili ajenda ya siasa za nje za kila siku za Marekani. Nchi hii itaamiliana kwa tahadhari na China na kujaribu kupunguza taathira za China katika eneo. 
Moja ya manowari za China
Pamoja na hayo yote, China inatambua vyema kuwa mipango ya kiuchumi ya Marekani ikiwemo ile ya kuongeza tozo ya ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka China na kuvibana vitega uchumi vya nchi hiyo inaweza kuisababisha madhara nchi hiyo. Ndio maana China nayo hivi karibuni ikaamua kuendeleza mipango yake ya ustawi wa kijeshi yaani kuimarisha uwezo wake wa kujilinda mkabala na  Marekani. Wakati huo huo China inaamini kuwa vita vikuu zaidi vya kulazimishwa dhidi yake kutoka kwa Rais Donald Trump ni vita vya kibiashara na mara kwa mara  imetahadharisha kuhusu madhara ya vita hivyo. 
Majeshi ya China yakifanya maneva kwenye maji ya kusini mwa nchi hiyo
Kwa vyovyote vile  Marekani inafahamu vyema kuwa China ni nchi pekee yenye ushawishi chanya mkabala na nafasi ya kimataifa ya Washington katika maeneo mbalimbali duniani. Suala hilo ndilo lililoifanya Marekani itekeleze siasa za pande zote katika nyanja za kijeshi na kiuchumi dhidi ya Beijing na katika upande wa pili pia serikali ya China inafanya kila iwezalo ili kudhibiti hali ya mgogoro na siasa hizo za Trump; siasa ambazo kwa mtazamo wa Beijing zimefanikiwa na zinaweza kuipelekea kuimarisha amani na usalama katika eneo la mashariki mwa Asia kwa kushirikiana nchi za eneo hilo.

Sunday, March 4, 2018

UN YASIMAMISH SHUGHULI ZAKE NIGERIA BAADA YA WAHUDUMU WAKE KUUAWA

UN yasimamisha shughuli zake Nigeria baada ya wahudumu wake kuuawa
Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kusitisha shughuli zake za utoaji huduma na misaada ya kibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na kuuawa wafanyakazi wake katika mashambulizi ya hivi karibuni ya magaidi wa Boko Haram.
Taarifa ya Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa, wahudumu 40 wa UN walikuwa katika mji wa Rann ambao una kambi ya wakimbizi wa ndani wapatao 55 elfu ulipovamiwa Alkhamisi usiku na wapiganaji wa Boko Haram.
Amesema kufuatia hujuma hiyo, Umoja wa Mataifa umesimamisha kwa muda utoaji wa huduma za kibinadamu katika mji huo ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram
Siku ya Ijumaa, shirika la madaktari wasio na mipaka lilitangaza habari ya kusimamisha shughuli zake zote kaskazini mwa Nigeria baada ya genge la wakufurishaji la Boko Haram kuushambulia mji wa Rann katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Katika shambulizi lililofanywa na genge hilo Alkhamisi usiku, watu 11 wakiwemo wafanyakazi watatu wa kutoa misaada waliuawa huku wengine watatu wakihofiwa kutekwa nyara baada ya hujuma hiyo.
Mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria na katika nchi jirani za Chad, Niger, na Cameroon yameshapelekea zaidi ya watu 20 elfu kuuawa na milioni mbili na laki sita wengine kuwa wakimbizi.

Friday, March 2, 2018

AL-SHABAAB YAUA ASKARI 5 WA KENYA KAUNTI YA MANDERA

Al-Shabaab yaua askari polisi 5 wa Kenya kaunti ya Mandera
Askari polisi watano wa Kenya wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kushambulia kambi mbili za maafisa usalama katika mji wa Fino katika kaunti ya Mandera.
Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Laafey huko kaskazini mwa Kenya, Eric Oronyi amesema shambulizi hilo limefanyika usiku wa kuamkia leo, ambapo wanamgambo hao wamevamia kituo cha polisi wa kawaida na wa utawala katika mji wa Fino.
Amesema wavamizi hao kati ya 70 hadi 100 mbali na kutekeleza mauaji hayo, kadhalika wameng'oa mlingoti wa shirika moja la simu za rununu na kulemaza mawasiliano.
Magaidi hao wamekuwa wakishambulia mabasi ya uchukuzi wa umma kaunti ya Mandera na kuua
Mwezi uliopita, maafisa wengine watano wa polisi ya Kenya waliuawa baada ya wanachama wa al-Shabaab kushambulia msafara wa magari ya maafisa usalama katika barabara ya Elwak-Kotulo katika kaunti hiyo hiyo ya Mandera.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye makao yake Somalia mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ndani ya ardhi ya Kenya kuishinikiza serikali ya nchi hiyo iondoe wanajeshi wake wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM