Thursday, November 16, 2017

WAMAREKANI WAZIDI KUPIGANA RISASI KIHOLELA, MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA

Wamarekani wazidi kupigana risasi kiholela, makumi wauawa na kujeruhiwa
Watu 16 wameuawa na wengine 24 kujeruhiwa katika matukio 56 ya kupigana risasi kiholela yaliyotokea katika kipindi cha masaa 24 kwenye maeneo tofauti ya Marekani.
Kituo cha kutoa takwimu za mashambulizi ya silaha nchini Marekani kimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa mauaji na mashambulizi hayo yametokea katika kipindi cha masaa 24 yaliyopoita katika majimbo ya Florida, Michigan, Texas, Ohio na Pennsylvania. 
Kwa mujibu wa kituo hicho cha Marekani, katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, kumeripotia matukio 164 ya kupigana risasi kiholela katika kona mbalimbali za Marekani ambayo yamepelekea watu 45 kuuawa na wengine 88 kujeruhiwa.
Umilikaji silaha ovyo, mgogoro mkubwa kwa Marekani

Takwimu zinaonesha kuwa, jamii ya Marekani ndiyo yenye silaha nyingi zaidi zinazomilikiwa na watu majumbani kuliko jamii nyingine yoyote duniani kiasi kwamba kati ya kila watu 100, 90 kati yao wana silaha nyepesi majumbani mwao.
Takwimu zinaonesha pia kuwa makundi ya utengenezaji silaha yana nguvu sana nchini Marekani na ndiyo yanayodhibiti vyama vya Democrats na Republican, hivyo serikali yoyote inayoingia madarakani haina nguvu ya kupiga marufuku umilikaji silaha ovyo nchini Marekani.

Wednesday, November 15, 2017

VYOMBO VYA HABARI MAGHARIBI VYANYAMANZIA KIMYA JINAI ZA SAUDIA DHIDI YA WAYEMEN

Vyombo vya habari vya Magharibi vyanyamazia kimya jinai za Saudia dhidi ya Wayemen
Wabunge nchini Iran wamelaani vikali mauaji yanayotekelezwa na Saudi Arabia dhidi ya raia wa Yemen huku wakisema jinai hizo zimenyamaziwa kimya na vyombo vya habari vya magharibi.
Katika taarifa siku ya Jumatano, wabunge 191 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran wamesema katika zama hizi ambazo, madola ya Magharibi, hasa Marekani, hudai kuwa watetezi wa haki za binadamu, tunashuhudia jinai za kuogofya zikitekelezwa na Saudi Arabia dhidi ya watu wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Yemen.
Wabunge wa Iran wametahadharisha kuwa Yemen inakabiliwa na maafa ya kibinadamu ambayo yamesababishwa na hujuma ya Saudia dhidi ya nchi hiyo sambamba na mzingiro wa anga, nchi kavu na bahari na hivyo kupelekea misaada ya dharura kama  dawa na chakuka kutowafikia Wayemen. Wabunge wa Iran wamesema Saudi Arabia na waitifaki wake, hasa Marekani, wanabeba dhima ya jinai dhidi ya watu wa Yemen.
Watoto ni waathirika wakuu wa jinai za Saudia nchini Yemen
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Swali kubwa hapa ni kuwa, je, ni vipi Saudi Arabia inawaua watu wasio na hatia kila siku kwa kutumia silaha mbali mbali hatari huku wanaodai kutetea haki za binadamu wakiwa kimya, bali hata wakiunga mkono jinai hizo?"
Wiki iliyopita Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alieleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kufunga kabisa mipaka ya Yemen kwa siku ya tano mfululizo na kusisitiza kuwa Yemen inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa duniani katika miongo ya hivi karibuni.
Saudi Arabia ikishirikiana na Marekani, Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Yemen Machi mwaka 2015. Maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi hayo.

NYUMA YA PAZIA LA MASHINIKIZO YA KUIONDOA IRAN NCHINI SYRIA

Nyuma ya pazia la mashinikizo ya kuiondoa Iran nchini Syria
Pamoja na kwamba Iran ni nchi iliyoko mstari wa mbele katika vita dhidi ya magaidi wakufurishaji nchini Syria, lakini waungaji mkono wa nyuma ya pazia wa magaidi wa Daesh (ISIS) hivi sasa wanafanya njama za kuhakikisha wanaandaa mazingira ya kurejea magaidi nchini humo kupitia kukabiliana waziwazi na kambi ya muqawama.
Siku chache zilizopita, Rex Tillerson, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisema: "Askari wa Iran, iwe ni wanajeshi wa Sepah au vikosi vinavyounga mkono na Iran, lazima viondoke katika ardhi ya Syria na kurejea makwao."
Akijibu madai hayo juzi Jumanne, Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia alisema kuwa, Iran iko kihalali nchini Syria na ni kwa ombi rasmi la serikali yenyewe ya nchi hiyo. Vile vile amekanusha uvumi wote ulioenezwa kwamba eti Moscow imeahidi kuwaondoa askari wa Iran nchini Syria.
Brigedia Jenerali Hossein Hamedani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi nchini Syria wakati akijitolea kutoa ushauri wa kijeshi wa kupambana na magenge ya kigaidi

Iran, Russia na Uturuki zimefanikiwa kupiga hatua kubwa katika utatuzi wa mgogoro wa Syria kupitia mazungumzo ya Astana na yumkini kama si mazungumzo hayo, leo hii magaidi wa Daesh (ISIS) wasingelikuwa wamedhoofishwa kiasi chote hiki.
Katika kukabiliana na mafanikio ya mazunungumzo hayo ambayo yamefanyika bila ya kushirikishwa upande wa Magharibi na Kiarabu ambao ni wa waungaji mkono wakuu wa magaidi huko Syria, upande huo umeamua kuishinikiza kambi halisi inayopambana na magaidi yaani Hizbullah ya Lebanon na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kama njia ya kuidhoofidha kambi ya muqawama na kuwarejesha magaidi katika eneo hili.
Matamshi ya kutaka walinzi wa Haram waondoke nchini Syria yametolewa katika hali ambayo, hadi hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba kuweko washauri wake wa kijeshi nchini Syria kumefanyika kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo kupambana na magaidi tena kwa ombi rasmi la serikali ya Damascus.
Lau kama Tehran ingelituma wanajeshi huko Syria kwa ombi la Russia au Marekani ni wazi kwamba suala la kuondoa askari hao lingelihitajia idhini ya moja kati ya nchi hizo. Lakini wakati nchi huru kama Iran ambayo si tegemezi kwa nchi nyingine yoyote inapoitikia ombi la serikali halali ya nchi fulani la kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo tena katika eneo hili, wakati huo hakuna nchi yoyote nyingine yenye haki ya kuitaka Tehran iondoke nchini humo.
Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia

Wale watu ambao hivi sasa wanapiga domo la kuitaka Iran iondoke Syria kwa madai kuwa magaidi wa Daesh wameshamalizwa nchini humo, wao ndio wanaopaswa kujibu ni kwa nini wana kambi zao za kijeshi katika eneo hili na kwa nini hawaondoi wanajeshi wao waliowamiminika katika kona mbalimbali za ukanda huu? Kwa mfano Washington inajigamba kuwa imelimaliza kundi la Taliban nchini Afghanistan baada ya kuwafurusha mjini Kabul na kwengineko, sasa kwa nini Marekani haiondoi kambi zake za kijeshi nchini humo bali kila leo inaongeza wanajeshi wake? Si hayo tu, lakini pia madola ya kibeberu kama Marekani yanapaswa kujibu ni kwa idhini ya nani yana wanajeshi na yanafanya mashambulizi ndani ya ardhi ya nchi huru ya Syria?
Ni jambo lililo wazi kwamba mashinikizo ya baada ya tawala za eneo hilo na mabwana zao wa nje ya ukanda huu, ya kuitaka Iran iondoke nchini Syria yanatokana na woga wao wa kuongezeka ushawishi wa Tehran katika fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu. Ushawishi huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio uliopelekea kuundika vikosi vya kujitolea vya wananchi katika nchi za Iraq, Syria na Yemen na ni jambo lililo bayana kwamba maadamu vikosi hivyo vya kujitolea vingalipo, Magharibi na vibaraka wao wenye fikra mgando hawataweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hili.

RUSSIA YATAHADHARISHA KUHUSU HATUA YA MAREKANI KWA VYOMBO VYAKE VYA HABARI

Russia yatahadharisha kuhusu hatua ya Marekani kwa vyombo vyake vya habari
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametangaza kuwa kila hatua itakayochukuliwai na Marekani dhidi ya waandishi habari na vyombo vya habari vya Russia haitaachwa bila ya jibu.
Dmitry Peskov amesema kuwa hatua yoyote itakayopelekea kubanwa uhuru wa vyombo vya habari vya Russia nje ya nchi haitasalia bila ya jibu; na kwamba hatua hiyo itafuatiliwa pia na fikra za waliowengi na kwa njia za kisheria.  
Dmitry Peskov, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia 
Katika fremu hiyo, Bunge la Russia (Duma) limepasisha mswada dhidi ya vyombo vya habari vya Marekani vinavyoendesha shughuli zake huko Russia. Bunge la Russia limetangaza kuwa, limechukua hatua hiyo kama jibu kwa hatua za karibuni za Marekani dhidi ya Televisheni ya Russia Today. Mwanasheria Mkuu wa Marekani siku kadhaa zilizopita aliitaka televisheni hiyo ya Russia Today iwe imejisali kama taasisi ya kigeni hadi kufikia tarehe 13 mwezi huu; kinyume chake akaunti za fedha za televisheni hiyo zilizopo Marekani zitafungwa.

SISITIZO LA UN LA ULAZIMA WA KUFUNGULIWA BANDARI YA AL HUDAYDAH NCHINI YEMEN

Sisitizo la UN la ulazima wa kufunguliwa bandari ya al Hudaydah nchini Yemen
Umoja wa Mataifa umepinga sharti lililotolewa na muungano vamizi wa nchi za Kiarabu unaofanya mauaji na umwagaji mkubwa wa damu nchini Yemen ambao umekataa kufungua bandari ya al Huydadah hadi pale matakwa yao ya kiuadui yatakapokubaliwa.
Kwa kweli hivi sasa hakuna watu wa nchi yoyote duniani walio na hali ngumu zaidi kushinda Wayemen. Hakuna mgogoro wowote ulioko duniani ambao hauko pia huko Yemen. Mashambulio ya kikatili ya Bani Saud ni ya kila siku nchini humo. Hakuna matumaini yoyote ya maisha nchini Yemen. Mabomu ya Aal Saud yanachukua roho za Wayemen kila siku huku njaa na magonjwa yakipigana vikumbo katika kuchukua roho za raia wasio na ulinzi wa nchi hiyo. Hali ni mbaya kiasi kwamba hata hakuna takwimu za kina za watu wanaokufa na kujeruhiwa kila leo katika nchi hiyo ya Kiislamu, lakini hata kama tutakubaliana na hizo hizo takwimu zinazotolewa na Umoja wa Mataifa basi tutaona ni kiasi gani Saudi Arabia na wenzake wanafanya ukatili wa kutisha katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa mujibu wa takwimu hizo, zaidi ya watu elfu nane wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Wahanga wa ukatili huo ni wa rika tofauti, kuanzia viajuza hadi vitoto vichanga, wanawake kwa wanaume. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema kuwa, kwa siku watu elfu saba wanaambukizwa ugonjwa wa kipindupindu na kila siku mamia ya raia wa nchi hiyo wanapoteza maisha. Njaa ni nduli wa tatu anayechukua roho za watu huko Yemen pembeni mwa vita na maradhi.
Hakuna waliosalimika na jinai za Saudi Arabia nchini Yemen
Mazingira ya hivi sasa yanasambaza harufu ya kifo kila sekunde nchini Yemen. Mgogoro wa nchi hiyo unakuwa mkubwa sekunde baada ya sekunde kutokana na nchi hiyo maskini kuzingirwa kila upande na kushambuliwa kila siku kwa kila aina ya silaha hata zilizopigwa marufuku. Hivi sasa njia zote za kuwafikishia misaada wananchi wa nchi hiyo zimefungwa. Hadi hivi sasa kumekuwa kukitolewa tahadhari za kutokea maafa makubwa ya kibinadamu ambayo yatakuwa makubwa zaidi duniani katika miongo kadhaa iliyopita. Lakini pamoja na hayo, na kutokana na uungaji mkono wa kila upande wa Marekani, serikali ya Saudia imekuwa ikipuuza tahadhari zote zinazotolewa. Mark Lukok, ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada ya kibinadamu. Alisema wiki iliyopita kwamba kama misaada ya binadamu haitafikishwa kwa wananchi wa Yemen haraka iwezekanavyo, basi ukame ambao haujawahi kutokea katika miongo kadhaa ya hivi karibuni duniani, utatokea nchini humo.
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Umoja wa Mataifa umeitaka Saudi Arabia kufungua haraka bandari ya al Hudaydah huko Yemen. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Bani Saud umekataa bali umezidi kung'ang'ania msimamo wake wa kuifunga kabisa bandari hiyo ambayo ndiyo njia pekee ya kuwafikishia misaada wananchi wa Yemen. Saudi Arabia inadai kuwa bandari hiyo ilikuwa inatumika kufanya magendo ya silaha nchini Yemen, lakini imeshindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kitendo cha Saudi Arabia cha kuifunga bandari hiyo ni ushahidi tosha kwamba ukatili wa wavamizi wa Yemen umeshindwa katika medani za vita na sasa wameamua kumalizia hasira zao kwa wananchi wa kawaida.
Licha ya ukatili mkubwa wanaofanyiwa, lakini wananchi wa Yemen bado wako ngangari, na wamesema katu hawatokubaliana na uvamizi wa nchi yao
Wachambuzi hao wanasema, hatua hiyo ya Saudia ni kujaribu kuishinikiza harakati ya Answarullah na waitifaki wake ili wakubali mapatano, baada ya kushindwa njama zote za maadui hao za kuidhibiti San'a, mji mkuu wa Yemen. Amma swali linalojitokeza habari ni kwamba, Umoja wa Mataifa ni mkweli kiasi gani katika mwito wake kwa Saudia wa kuitaka ifungue bandari ya al Hudaydah huko Yemen? Inabidi tusubiri na kuona ni kiasi gani umoja huo utaweza kuushinikiza ukoo wa Aal Saud katika suala hilo ndipo tutakapoweza kujua ukweli wa Umoja wa Mataifa katika mwito wake huo.

RAIS ROBERT MUGABE WA ZIMBABWE AONDOLEWA MADARAKANI

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aondolewa madarakani
Jeshi la Zimbabwe limemuondoa madarakani rais wa nchi hiyo Robert Gabriel Mugabe.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters jeshi limetangaza kuwa Mugabe na familia yake wako kwenye kizuizi cha nyumbani na kuongeza kuwa jeshi hilo litawapandisha kizimbani wale liliowataja kama "wahalifu" waliomzunguka kiongozi huyo ambao wamesababishia madhara na hasara za kiuchumi na kijamii nchi hiyo.
Sambamba na hayo ofisi ya rais wa Afrika Kusini imetangaza kuwa Mugabe mwenyewe amezungumza kwa njia ya simu na rais wa nchi hiyo Jacob Zuma na kumueleza kwamba amezuiliwa nyumbani kwake lakini yuko salama.
Duru za serikali zimeripoti kuwa Waziri wa Fedha Ignatius Chombo ambaye ni mmoja wa viongozi wa mrengo unaojulikana kama G40 unaomuunga mkono mke wa Mugabe Bi Grace amewekwa kizuizini na jeshi.
Grace Mugabe
Imeelezwa kuwa hatua ya jeshi kuingilia kati masuala ya kisiasa na uongozi nchini Zimbabwe imelenga kumzuia Rais Mugabe kumfanya mkewe Grace mrithi wa urais baada yake.
Aliyekuwa makamu wa rais wa Zimbabwe  Emmerson Mnangagwa amesema hakuna mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo na kwamba mchakato wa mapokezano ya madaraka umo katika hali ya kufanyika pasi na kutokea umwagaji damu wowote.
Hayo yanajiri huku chama kikuu cha upinzani cha MDC kikitoa wito wa kurejeshwa demokrasia nchini kwa msingi wa kuheshimu katiba.
Askari wa jeshi wakiwa kando ya magari ya deraya kandokando ya mji wa Harare
Chama hicho kimeeleza kuwa kina matumaini kwamba uingiliaji kati wa jeshi utapelekea kuundwa serikali ya kidemokrasia, yenye uthabiti na ya kuiletea Zimbabwe maendeleo.
Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na Mugabe mwenye umri wa miaka 93 ya kumuuzulu  makamu wake Emmerson Mnangagwa iliitumbukiza Zimbabwe kwenye mgogoro na mvutano ambao haujawahi kushuhudiwa.
Hapo jana jeshi lilichukua hatua, kwanza ya kulidhibiti jengo la televisheni ya taifa na kisha kusambaza magari mengi ya deraya katika barabara za kandokando ya mji mkuu Harare.
Jeshi la Zimbabwe limechukua hatua hiyo huku kamanda wake mkuu akiwa ameshaonya hapo kabla kwamba wanajeshi wanaweza kuchukua hatua ya kuingilia kati endapo mwenendo wa kuwauzulu na kuwavua nyadhifa zao viongozi ndani ya chama tawala ZANU-PF utaendelea.../

Wednesday, November 8, 2017

MAANDAMANO MENGINE YAZUKA CATALONIA

Mahakama ya katiba ya Uhispania imetoa maamuzi kwamba kura ya bunge la Catalonia ya hivi karibuni ya kutangaza uhuru kutoka Uhispania ilikuwa kinyume cha sheria. 
 Maamuzi hayo yaliyotolewa leo yamekuja wakati kuna maandamano makubwa ya wanaounga mkono kujitenga waliofunga barabara na njia za treni kama sehemu ya kugomea kufungwa kwa maafisa wa serikali ya Catalonia na wanaharakati wanaopigania kujitenga kabla na baada ya azimio la Oktoba 27.
 Mahakama imeanza kwa kusimamisha utekelezaji wa azimio la kujitenga la mwezi uliopita wakati ikiangazia uhalali wake kutokana na kupingwa na serikali ya Uhispania.
  Zaidi ya barabara 50 ikiwa ni pamoja na barabara kuu zilifungwa na kusababisha usumbufu mkubwa katika jimbo hilo linalokabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na hatua ya serikali yake kutaka kujitenga na Uhispania. Mzozo huo umeutikisa Umoja wa Ulaya unaosaka suluhu kufuatia hatua ya ghafla ya kujitoa kwa Uingereza na kuzua hofu ya machafuko na usumbufu usiokwisha kwenye taifa hilo.