Wednesday, November 8, 2017

TRUMP AWASILI CHINA

Rais wa Marekani, Donald Trump amewasili China ambapo atakutana na Rais wa nchi hiyo Xi Jinping, huku ajenda kuu ya mazungumzo yao ikiangazia zaidi mzozo wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini na masuala ya kibiashara.
China Trump auf erster Asien-Reise (picture-alliance/AP Photo/A. Harnik) Donald Trump na Xi Jingping wakiwa na wake zao
Trump amewasili leo kwenye mji mkuu wa China, Beijing akiwa na mkewe Melania na kupokelewa kwa bendi ya jeshi kabla ya kuelekea Forbidden City ambako kuna makumbusho ya kasri la kifalme, mji ambao anakutana na Rais Xi pamoja na mkewe Peng Liyuan.
Saa chache kabla ya kuwasili mjini Beijing, Trump aliitolea wito China kusaidia katika kukabiliana na uchokozi unaofanywa na Korea Kaskazini kutokana na mpango wake wa nyuklia. Ikulu ya Marekani imesema Trump ataitumia ziara hiyo kuiomba China kusitisha uhusiano wake wa kifedha na Korea Kaskazini na kuheshimu vikwazo vya Umoja wa Mataifa. China ni mshirika mkubwa wa kibiashara na Korea Kaskazini.
Akiwa Korea Kusini kiongozi huyo wa Marekani alizitaka China na Urusi kusaidia kuiwekea shinikizo Korea Kaskazini kusitisha kutengeneza silaha za nyuklia na kuileta nchi hiyo katika meza ya mazungumzo. Akizungumza katika Bunge la Korea Kusini mjini Seoul, Trump ametoa onyo kali kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ambapo amemtaka asiwadharau na wala asiwajaribu.
''Hatuwezi kuruhusu Marekani au washirika wetu kushambuliwa. Hatuwezi kuruhusu miji ya Marekani itishiwe na silaha za maangamizi. Hatutoogopa. Na hatutoruhusu ukatili mwingine ujirudie katika historia, kwenye ardhi hii ambayo tuliipigania na kufa kwa ajili ya kuilinda,'' alisema Trump.
Südkorea Seoul Trump spricht in der Nationalversammlung (Reuters/J. Ernst) Trump akilihutubia bunge la Korea Kusini
Rais Trump amezitaka Urusi na China kusitisha uhusiano wowote na Korea Kaskazini, ukiwemo ule wa kidiplomasia. Aidha, amesema muda wa kutoa sababu na visingizio umekwisha na kwamba sasa ni wakati wa kuwa imara, kwani mtu anayetaka amani lazima asimame imara wakati wote.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesisitiza kwamba nchi hiyo imewahi kutekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Korea Kaskazini, lakini imesema itachunguza iwapo kuna shughuli ambazo zinakiuka maazimio hayo. Kwa mujibu wa wizara hiyo, China bado ina matumaini ya kuutatua mzozo uliopo kwa njia ya mazungumzo.
Kwa upande wa masuala ya kibiashara, Trump bado yuko katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashirika ya biashara ya Marekani katika kutatua malalamiko ya kibiashara na China. Marekani imeishutumu China kwa kurudia ahadi yake ya kufungua masoko yake. Wiki iliyopita Trump alisema kulikuwa na hasara ya kibiashara ya Dola bilioni 347 kati ya nchi hiyo na China na kwamba hatua hiyo ni mbaya na inatia aibu. 
China ni kituo cha tatu cha ziara ya siku 12 ya Trump barani Asia ambayo itamfikisha pia Vietnam na Ufilipino. Tayari kiongozi huyo wa Marekani ameizuru Japan na Korea Kusini.

MWANAMFALME: HAKI ZA BINADAMU ZINAKANYAGWA SANA SAUDIA

Mwanamfalme: Haki za binadamu zinakanyagwa sana Saudia
Khalid bin Farhan Al Saud, Mwanamfalme ambaye amejitenga na utawala wa Aal-Saud, amesema kuwa kabla ya kuomba hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani, kwa muda mrefu alikuwa akiishi kwa wasiwasi na mashaka mengi nchini Saudia.
Farhan Al Saud ambaye ni mpinzani wa utawala wa Saudia ameyasema hayo katika mahojiano na kanali moja ya televisheni ya Ujerumani ambapo amezungumzia kutokuwepo uhuru wa kujieleza na ukiukwaji haki za binadamu uliokithiri nchini humo. Amesema kuwa, baada ya kupinga utawala wa Aal-Saud na kuwasilisha malalamiko ya kuwepo uhuru wa kiraia, alikumbwa na mashinikizo na udhia mkubwa kiasi kwamba alilazimika kujiuzulu jeshini na kutoroka nchi.
Khalid bin Farhan Al Saud, Mwanamfalme wa Saudia
Mwanamfalme huyo wa utawala wa Aal-Saud sambamba na kusisitiza kuwa, haogopi kitu chochote amesema zaidi ya mapendekezo 50 yamewasilishwa kwake kutoka ubalozi wa Saudia nchini Ujerumani yakimtaka aandike taarifa ya kuomba msamaha kwa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud lakini amekataa kufanya hivyo. Khalid bin Farhan Al Saud ameashiria pia njama za viongozi wa Saudia za kumuwekea mashinikizo na hata ikiwezekana kumtia mbaroni kwa kumtumia dada yake anayeitwa 'Ibtisam' na anaeshikiliwa katika kifungo cha nyumbani nchini Saudia na kusema kuwa, watawala wa ukoo wa Aal-Saud kwa mara kadhaa walimtisha kwamba ikiwa hatoacha kufichua machafu ya utawala wa kifalme wa Saudia, watamuua dada yake.
Ukandamizaji wa askari wa Aal-Saud
Kwa mujibu wa takwimu na ripoti za ndani nchini Saudia, zaidi ya wanaharakati wa kisiasa na wanasheria elfu 30 wanashikiliwa katika jela mbalimbali za utawala huo wa Aal-Saud.

AMISOM KUONDOA ASKARI 1,000 NCHINI SOMALIA

AMISOM kuondoa askari 1,000 nchini Somalia
Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) umetangaza kuwa utaondoa askari 1,000 kutoka Somalia hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, Francisco Madeira amesema kuwa AMISOM imeanza kupunguza idadi ya askari wake nchini humo na kwamba kufikia tarehe 31 Disemba askari 1000 wa kikosi hicho watakuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.
Madeira amesisitiza umuhimu wa kuwepo umoja kati ya raia na jeshi nchini Somalia dhidi ya ugaidi na kusema jeshi peke yake haliwezi kuwashinda magaidi bila ya msaada ya raia. Amewataka Wasomalia wote kushirikiana kwa ajili ya kuwafukuzia mbali wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab. 
Kikosi cha majeshi ya Umoja wa Afrika cha AMISOM ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007. 
Askari wa kikosi cha AMISOM, Somalia
Kikosi hicho kinaundwa na askari elfu 22 kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopita.
Magaidi wa al Shabab wamezidisha mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu katika wiki za hivi karibuni husuan katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. 

KENYA YAPINGA HATUA YA TANZANIA KUPIGA MNADA ZAIDI YA NG' OMBE 1,300

Kenya yapinga hatua ya Tanzania kupiga mnada zaidi ya Ng’ombe 1,300
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed ameilalamikia serikali ya Tanzania kufuatia hatua ya taifa hilo kuwapiga mnada zaidi ya ng’ombe 1,300 walioingia nchini humo kinyume na sheria.
Serikali ya Rais John Magufuli ilichukua hatua hiyo baada ya wafugaji kuingia nchini humo na mifugo yao wakitafuta lishe.
Hatua hiyo imekuja siku moja tu baada ya Rais Magufuli kusema kuwa taifa hilo sio shamba la mifugo wa taifa jirani.
Akizungumza katika mkoa wa Kagera ambako alikuwa katika ziara yake ya kikazi Magufuli alisema kwamba Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani na kwamba ataichukulia mifugo hiyo hatua kali za kisheria. 
Rais wa Tanzania John Magufuli
Vilevile alizitaka nchi Jirani kuchukua hatua kama hiyo iwapo mifugo ya Tanzania wataingia katika mataifa hayo kinyume na sheria.
Hatua ya kuwapiga mnada ng’ombe hao imezua hisia kali miongoni mwa wafugaji wa Kenya baada ya wenzao waliokuwa na mifugo hao kukamatwa na kuzuiliwa kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed amenukuliwa akisema: ”Tulidhani kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yangetatua mzozo huu, lakini tumeshindwa kufikia makubaliano.
Amesema: ”Historia ambayo tumekuwa nayo na Watanzania ni nzuri sana na kila kunapotokea tatizo tumekuwa tukitatua. Ni kwa sababu hiyo ambapo imekuwa hatua ya kushangaza miongoni mwa wafugaji wa Kenya”,
Bi Mohamed amesema kuwa Kenya imekuwa ikiwavumilia wafugaji wa nchi jirani ambao wamekuwa wakivuka mara kwa mara na kuingia katika eneo la Kajiado nchini Kenya.

Saturday, November 4, 2017

MALENGO YA HATUA YA KIJESHI LA MAREKANI NCHINI SOMALIA

Malengo ya hatua za kijeshi za Marekani nchini Somalia
Kutokana na kushadidi mashambulizi ya kigaidi katika ardhi ya Somalia, ndege za kivita za Marekani kwa mara ya kwanza zimefanya mashambulizi dhidi ya ngome za makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.
Kundi la kigaidi la al Shabab ambalo limetangaza utiifu wake kwa viongozi wa kundi la al Qaida limekuwa likipigana na serikali ya Somalia kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hilo liliteka miji kadhaa ya Somalia ikiwemo sehemu kubwa ya mji mkuu Mogadishu lakini Agosti mwaka 2011 lilifurushwa katika miji na maeneo mengi ya nchi hiyo kutokana na mashambulizi makubwa ya jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika. Hata hivyo kundi hilo la kigaidi bado linadhibiti miji kadhaa hususan maeneo ya vijijini ya Somalia. 

Wanamgambo wa kundi la al Shabab wenye makao yao Somalia 
Katika miezi ya hivi karibuni kundi hilo limebadili mbinu zake kwa kuzidisha mashambulizi ya kuvizia na kujilipua kwa mabomu badala ya kukabiliana moja kwa moja na vikosi vya jeshi la serikali ya Somalia na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni shambulizi la wiki mbili zilizopita mjini Mogadishu ambalo limeua karibu watu mia nne. 
Kwa sasa Marekani, kama kawaida yake, imeparamia wimbi la kupambana na ugaidi na kundi la al Shabab na kuanza kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya Somalia kwa kushambulia baadhi ya maeneo ya kundi hilo. Tunapotupia jicho sera na siasa za Marekani barani Afrika tunaona kuwa, japokuwa askari wa Marekani wamekuwepo kwa miaka mingi katika nchi mbalimbali za Afrika lakini nchi hiyo ilianzisha rasmi kambi na eneo lake la sita la kijeshi duniani mwaka 2007 kwa kuanzisha ofisi ya Komandi ya Jeshi ya Marekani Barani Afrika AFCOM kwa kifupi. Katika kipindi cha miaka kadhaa ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikichunga na kufuatilia harakati zote za kijeshi barani Afrika na kufuatilia maslahi yake haramu katika nchi za bara hilo kwa kutumia njia na mbinu mbalimbali kama kutuma washauri wa masuala ya kijeshi na eti kutoa mafunzo kwa majeshi ya nchi za Kiafrika. Miongoni mwa malengo hayo yanayohudumia maslahi ya Marekani ni kufuatilia harakati za nchi wapinzani kama China na Russia huko Afrika, kufuatilia maslahi ya kiuchumi na kibiashara na kutumia maeneo ya kistratijia ya nchi za bara hilo kwa malengo ya kikoloni.  
Mchambuzi Nick Turse anasema: Kwa sasa Marekani ina vikosi vya jeshi katika nchi kadhaa za Afrika ambazo hazina tatizo lolote la makundi ya kigaidi kama lile la Daesh. Kwa msingi huo hatuwezi kusema kuwa operesheni zinazofanywa na wanajeshi hao wa Marekani ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugaidi kama wanavyodai viongozi wa serikiali ya Washington".
Pamoja na hayo Marekani imezidisha kasi ya kutuma majeshi yake barani Afrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi kama inavyoshuhudiwa katika nchi kama Niger. Operesheni hizo zinaipa Marekani fursa ya kutimiza malengo yake ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Seneta Lindsay Graham wa Kamati ya Jeshi la Marekani anasema: Maana na hakika ya vita imo katika hali ya kubadilika na sasa tunashuhudia hatua zaidi barani Afrika.
Alaa kulli hal, ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, Washington ni miongoni mwa pande zilizoshiriki kuunda na kuanzisha makundi hatari ya kigaidi kama Daesh, Al Qaida na Twaliban. Hivyo basi mashambulizi ya sasa dhidi ya wapiganaji wa al Shabab ni ya kimaonyesho tu yanayofanyika kuwahadaa walimwengu au kwa shabaha ya kutimiza malengo ya kikoloni ya nyuma ya pazia.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh 

MAPIGANO YAENDELEA KASKAZINI MWA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Mapigano yaendelea kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imeripoti kuwa mapigano makali yangali yanaendelea katika mkoa wa Ouham kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo ya kimataifa ya tiba, mbali na kueleza wasiwasi uliopo kutokana na kuendelea mapigano yaliyochanganyika na vitendo vya ukatili kwenye maeneo mabalimbali ya mkoa wa Ouham imeongeza kuwa watu wasiopungua wawili waliuawa na wengine 21 walijeruhiwa katika mapigano yaliyotokea wiki iliyopita baina ya makundi mawili hasimu.
Kwa mujibu wa duru zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa mapigano hayo yalihusisha kundi la waasi wa Kikristo la Anti-Balaka na wanamgambo wa kundi la wabeba silaha liitwalo Harakati ya Kizalendo kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (MPC) ambalo limeundwa na baadhi ya waasi wa zamani wa harakati ya Seleka.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikishuhudia mapigano na machafuko tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo François Bozizé alipoondolewa madarakani Machi 24, mwaka 2013 na harakati hiyo.
Rais Faustin-Archange Touadéra
Licha ya kufanyika uchaguzi wa rais mnamo mwezi Machi mwaka uliopita wa 2016 uliomleta madarakani rais wa sasa Faustin-Archange Touadéra, hata hivyo serikali ya Bangui inayoongozwa na kiongozi huyo hadi sasa imeshindwa kurejesha amani na uthabiti nchini humo.
Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipofanya safari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katikati ya mwezi uliopita wa Oktoba aliashiria kuwa anakusudia kutoa wito wa kuongezwa askari wa ziada 9,000 katika operesheni za kulinda amani nchini humo hasa kwa ajili ya kuwalinda raia.../

Thursday, November 2, 2017

RAIS MUGABE ATAKA KUREJESHWA HUKUMU YA KIFO NCHINI ZIMBABWE

Rais Mugabe ataka kurejeshwa hukumu ya kifo nchini Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametoa mwito wa kurejeshwa hukumu ya kifo baada ya watu 50 kutuma maombi ya kujaza nafasi iliyo wazi ya mtu wa kutekeleza adhabu ya kunyongwa.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, Mugabe ametoa wito huo hii leo Alkhamisi katika mji mkuu Harare, wakati wa mazishi ya veterani mashuhuri aliyepigania uhuru wa nchi hiyo ambapo ameongeza kuwa, "Nahisi kuna haja turejeshe hukumu ya kifo. Watu wanacheza na kifo kwa kuteleleza mauaji ya kiholela."
Hukumu ya kifo ambayo ipo katika vitabu vya sheria ya nchi hiyo haijatekelezwa tangu mwaka 2005, baada ya mtu aliyekuwa akitekeleza adhabu hiyo kuaga dunia.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Amnesty International yamekuwa yakiitaka Zimbabwe ipige marufuku hukumu ya kifo, ambayo inawakabili wafungwa 92.
Rais Mugabe wa Zimbabwe
Mugabe mwenye umri wa miaka 93 amekuwa akiiongoza Zimbabwe, koloni la zamani la Uingereza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1980.
Baadhi ya wakosoaji wa serikali ya Zimbabwe wamekuwa wakimuona Mugabe kama kiongozi dikteta mwenye kuiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma, huku akiwa na kauli ya mwisho kwenye mihimili yote ya serikali.