Saturday, September 16, 2017

HUFFINGTON POST: WAMAREKANI NI WABAGUZI

Matokeo ya uchunguzi wa taasisi mbili za kisayansi za Marekani yanaeleza kuwa, watu wengi wa nchi hiyo wana mielekeo ya kibaguzi licha ya kutoa madai ya kupinga fikra ya kuwatambua wazungu kuwa ndio wanadamu walio juu na bora kuliko wengine.
Gazeti la Huffington Post linalochapishwa nchini Marekani limeripoti kuwa, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na taasisi ya Ipswich na Chuo Kikuu cha Virginia yameonesha kuwa, ingawa idadi ya waungaji mkono wa manazi mamboleo na fikra kwamba wazungu wako juu na ni bora zaidi kuliko wanadamu wengine, lakini baadhi ya fikra na mitazamo ya kibaguzi na ya kufurutu mipaka inaungwa mkono kwa wingi nchini humo. 
Uchunguzi huo wa maoni ulifanyika kuanzia tarehe 21 Agosti hadi tarehe 5 Septemba, yaani wiki kadhaa tu baada ya mapigano ya wabaguzi wa rangi katika jimbo la Virginia.
Maandamano ya kupinga ubaguzi nchini Marekani
Matokeo ya uchunguzi huo pia yameonesha kuwa, asilimia 8 ya washiriki wamesema kuwa, wanaiunga mkono harakati ya kitaifa ya wazaungu wabaguzi na kwamba asilimia 39 kati yao wanaamini kuwa, wazungu wanashambuliwa nchini Marekani!
Uchunguzi huo umebaini kuwa, mtu mmoja kati ya kila Wamarekani sita anaamini kwamba, ndoa zinapaswa kufanyika baina ya watu wa mbari moja na si kwa mfano kati ya Wamarekani weusi na wazungu.  
Kyle Kondick Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kisiasa wa Chuo Kikuu cha Virginia anasema matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa, jamii ya Marekani ina mitazamo inayokubali ubaguzi wa rangi.    

IRAN; MOJAYA MADOLA MANNE YANAYOONGOZA KATIKA TEKNOLOJIA YA SATALAITI DUNIANI

Nguvu na uwezo wa kielimu sambamba na nguvu za kiulinzi na makombora ni miongoni mwa mambo muhimu yanayojenga nguvu na uwezo wa taifa lolote katika zama hizi; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa upande wake imepiga hatua nzuri katika uga wa nguvu na uwezo wa kielimu na kisayansi hususan katika teknolojia ya satalaiti.
Mshauri wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza siku ya Alkhamisi kuwa: Iran ni moja ya nchi nne duniani zinazoongoza katika nyanja zote za teknolojia ya satalaiti. Brigedia Jenerali Mohammad Hassan Nami amesema Iran inao utaalamu na uwezo mkubwa katika nyuga za teknolojia ya satalaiti ikiwemo vituo vya kurushia, mitambo ya kubebea angani, satalaiti zenyewe pamoja na vituo vya upokeaji na uongozaji.
Brigedia Jenerali Mohammad Hassan Nami
Mafanikio katika uga wa kutuma satalaiti angani sambamba na uwezo wa kuunda makombora ya aina mbalimbali yenye uwezo na malengo tofauti yameifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwe na nguvu na uwezo katika nyanja za aina kwa aina. Kutengeza satalaiti na kuituma anga za mbali kwa kutumia maroketi ya kubebea satalaiti ni upeo wa juu kabisa wa utunishaji nguvu na misuli ya uwezo wa nchi yoyote ile katika uga wa teknolojia ya anga za mbali. Katika uwanja huo, Iran imetuma angani satalaiti mbalimbali kwa kutumia maroketi ya kubebea satalaiti; na hivi sasa ni miongoni mwa nchi nne zinazoongoza katika uga huo duniani ikiwa pia imo kwenye mikakati ya kutuma wanadamu katika anga za juu. Akizungumzia suala hilo, Fat-hollah Ummi, Mkuu wa kituo cha utafiti wa anga za mbali cha Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran alitangaza wiki iliyopita kwamba: "marubani wanne wenye uzoefu mkubwa hivi sasa wanapatiwa mafunzo makubwa na magumu ili hatimaye wawili miongoni mwao wachaguliwe kwa ajili ya kutumwa kuelekea anga za mbali".
Satalaiti ya Omid iliyotumwa na Iran katika anga za mbali
Kabla ya hapo, mnamo mwaka 2013, wanasayansi wa anga za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walifanikiwa kutuma anga za mbali kima wawili waliopewa majina ya Aftab na Fargam; na kwa mujibu wa Fat-hollah Ummi hadi sasa kima hao wawili wangali hai; na wataalamu wa Kiirani wanafanya utafiti kuhusu athari za safari za anga za mbali kwa mtoto aliyezaliwa na kima hao.
Kwa kutegemea uwezo na utaalamu wake wa ndani na juhudi za waatalamu wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kuwa moja ya mataifa yenye uwezo wa juu katika nyuga mbalimbali za teknolojia ya satalaiti. Kutokana na mafanikio makubwa iliyopata, kila pale inapotuma satalaiti kwa mafanikio kuelekea anga za mbali, maadui zake wakiongozwa na Marekani hushindwa kuvumilia jambo hilo. Kwa kutoa mfano, mnamo tarehe 27 Julai mwaka huu, Iran ilifanikiwa kurusha kwa mafanikio roketi la kubebea satalaiti la Simorgh katika kituo cha taifa cha anga za mbali cha Imam Khomeini (MA) kilichopo hapa mjini Tehran. Siku moja tu baada ya mafanikio hayo, yaani tarehe 28 Julai, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitumia kisingizio cha kufanyiwa jaribio roketi la Simorgh ambalo lilihusu masuala ya utafiti tu na kisayansi, kuzijumuisha taasisi sita za Iran kwenye orodha ya vikwazo vyake dhidi ya taifa hili. Katika hatua nyengine inayofanana na hiyo, Alkhamisi ya tarehe 14 ya mwezi huu wa Septemba wizara hiyo iliongeza majina ya watu na mashirika mengine kadhaa ya Kiirani yanayohusika na masuala ya makombora kwenye orodha ya vikwazo dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya serikali ya Washington inakinzana na sheria za kimataifa na hata makubaliano ya nyuklia na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Akizungumza siku tatu zilizopita pembeni ya mkutano wake na Katibu Mkuu wa Shirikia la Ushirkiano wa anga za mbali la Asia na Oceania (APSCO), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia za Mawasiliano wa Iran Mohammad Javad Azari Jahrami alisema: "Sekta ya anga za mbali haikuashiriwa kwa namna yoyote ile kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na hata katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama pia sekta ya satalaiti ya Iran haijawekewa mpaka wowote".
Rais Hassan Rouhani alipokagua uundaji wa roketi la Simorgh
Shughuli za satalaiti na utumaji wake kuelekea anga za mbali kwa malengo ya utafiti ni jambo la dharura na la kawaida kwa nchi yoyote ile. Kwa sababu hiyo, bila kujali hatua za kutapatapa zinazochukuliwa na Marekani, Iran ingali inaendelea kupiga hatua na kusonga mbele katika uga huo ambapo hivi sasa inajiandaa kutuma anga za mbali satalaiti nyengine mpya iliyopewa jina la "Satalaiti ya Urafiki". Kuwa na nguvu na uwezo katika sekta mbalimbali kumeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwe dola athirifu na lenye sauti katika eneo na ulimwenguni kwa jumla, ambapo licha ya kuandamwa na mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi hivi sasa imekuwa moja ya madola yanayoongoza katika uga wa utaalamu wa makombora na satalaiti duniani.../

WAAFRIKA KUSINI WAANDAMANA KUPINGA MAUAJI YA KIMBARI YA WAISLAMU, MYANMAR

Wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano wakilaani mauaji ya kimbari yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Waandamanaji hao waliokusanyika mbele ya ubalozi wa Myanmar mjini Pretoria walikuwa wakipinga nara za kutaka kukomeshwa mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya. 
Maulana Bham ambaye ni mjumbe wa Baraza la Waislamu nchini  Afrika Kusini alisema katika maandamano hayo kwamba, walimwengu wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya umati yanayofanyika dhidi ya Waislamu nchini Myanmar. 
Mauaji yanayofanywa na Mabudha wa Myanmar wakishirikiana na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya yameamsha hasira na malalamiko katika nchi mbalimbali duniani. 
Maiti za Waislamu wa Rohingya
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya Waislamu laki nne wa Rohingya wamelazimishwa kuhama makazi yao na kukimbilia Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi uliopita wa Agosti kutokana na ukatili na mauaji yanayofanywa na Mabudha. Waislamu wengine zaidi ya elfu sita wameuawa na wengine elfu 8 wamejeruhiwa. 
Ukatili mkubwa zaidi dhidi ya Waislamu nchini Myanmar unafanyika katika mkoa wa Rakhine ulioko magharibi mwa nchi hiyo. 

Wednesday, September 13, 2017

KUENDELEA KUKOSOLEWA SIASA TRUMP KUHUSIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Katika hali ambayo kimbunga cha Irma bado kinaendelea kuyakumba maeneo kadhaa ya Marekani, baadhi ya duru za kisiasa na vyombo vya habari nchini humo vimeonyesha wasi wasi wao kuhusiana na siasa za Rais Donald Trump katika uwanja wa mabadiliko ya tabianchi.
John McCain, seneta wa chama cha Republican amekosoa vikali msimamo wa Rais Donald Trump kuhusiana na suala hilo. Akizungumza katika mahojiano maalumu, McCain amesema kuwa, hivi sasa dunia inashuhudiwa mabadiliko ya hali ya hewa ambayo hayajawahi kushuhudiwa huko nyuma. Amesisitizia umuhimu wa kutumiwa nyuklia kama chanzo salama cha nishati safi kuliko siasa za Trump, zinazosisitiza juu ya utumiwaji wa nishati ya mafuta.
John McCain
Amesema kuwa, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuna udharura wa kuchukuliwa hatua ambazo hazitowadhuru raia wa kawaida. Matamshi ya John McCain yametolewa katika hali ambayo katika wiki mbili zilizopita Marekani imekuwa ikishuhudia vimbunga vikali cha hivi karibuni zaidi kikiwa ni kimbunga cha Irma katika jimbo la Florida ambacho kimesababisha uharibifu mkubwa jimboni humo. Kabla ya hapo pia yaani mwezi Agosti, wakazi wa majimbo ya Texas na Louisiana walishuhudia kimbunga kingine cha Harvey ambapo sambamba na kusababisha uharibifu mkubwa unaokadiriwa kuwa wa dola bilioni 180, zaidi ya watu 60 walipoteza maisha katika kimbunga hicho. Ripoti iliyotolewa na serikali ya Washington inaonyesha kwamba, mabadiliko ya tabianchi yanayoshuhudiwa duniani hivi sasa, yanaufanya mwaka jana wa 2016 kuwa mwaka uliokuwa na joto jingi zaidi katika miongo kadhaa ya hivi karibuni. Wataalamu wa mambo wameonya kwamba, hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa wa mjini Paris, Ufaransa, inaweza kusababisha ongezeko kubwa la joto na uharibifu wa hali ya hewa duniani.
Rais  Donald Trump wa Marekani
Pamoja na hayo, lakini bado Rais Donald Trump anaendelea kupuuza suala la mabadiliko ya tabianchi ambapo sambamba na kufumbia macho indhari za wataalamu, tarehe 20 Januari mwaka huu alitangaza kuiondoa nchi yake katika Mkataba Mazingira wa Paris. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, vimbunga vya Harvey na Irma vimeongeza mashinikizo dhidi ya serikali ya Marekani kutokana na kufumbia kwake macho tahadhari zinazotolewa juu ya taathira hasi za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mtazamo wa weledi wa mambo, Trump hapaswi kufanya ujeuri unaompelekea kupinga uchunguzi na utafiti unaofanywa na wataalamu wa taaluma tofauti na hasa wa masuala ya mazingira. Katika uwanja huo Noam Chomsky, msomi na mkosoaji mashuhuri wa Marekani anaamini kwamba, Rais Donald Trump anakusudia kuiangamiza dunia.
Vimbunga vikali vnavyoendelea kuikumba Marekani 
Baada ya kutangazwa hali ya hatari katika jimbo la Florida, Tomás Pedro Regalado, Meya wa mji wa Miami alisema kuwa, sasa umefika wakati wa kufanya uchunguzi na mazungumzo kuhusiana na suala zima la tabianchi na Trump kwa kushirikiana na Wakala wa Kulinda Mazingira wa nchi hiyo ili kuchukua maamuzi muhimu kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa. Hata kama hadi sasa haijafahamika wazi ikiwa ni mabadiliko ya tabianchi ndiyo yamepelekea kuongezeka vimbunga vya mwaka 2017 nchini Marekani na katika maeneo mengine ya duania au la, lakini wataalamu wa mambo wanaamini kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba vimbunga hivyo huenda vikawa vimeathiriwa moja kwa moja na mabaliko ya hali ya hewa duniani. Ukweli ni kwamba, ikiwa Rais Donald Trump na serikali yake wataendelea kupinga ukweli kwamba mabadiliko ya tabianchi na taathira zake ndicho chanzo cha vimbunga vinavyoshuhudiwa hii leo, basi maisha ya mamilioni ya Wamarekani yatakuwa katika hatari kubwa.

POLISI KENYA YATUMIA GESI YA KUTOA MACHOZI BAADA YA WANAWAKE KUVAMIWA MUKUTANONI

Polisi nchini Kenya katika mji wa Kisumu magharibi mwa nchi hiyo leo wamenyunyiza angani gesi ya kutoa macho na kufyatua risasi ili kuwatawanya vijana wa kiume waliovamia hoteli moja na kuanza kuwapiga wanawake waliokuwa wakihudhuria mkutano wa uchaguzi mjini humo.
Tarehe Nane mwezi Agosti mwaka huu Kenya ilifanya chaguzi za Rais, bunge na serikali za mitaa, hata hivyo wiki tatu baadaye mahakama ya juu ya nchi hiyo ilitengua matokeo ya uchaguzi wa rais ikiashiria kuwepo kasoro na dosari katika mfumo wa utoaji matokeo. Uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika Oktoba 17 mwaka huu.
Jumuiya ya Wanawake wa Kikristo ya Kenya leo Jumatano ilikuwa ikifanya mkutano wake kuhusu marudio ya uchaguzi huo tajwa mara ikivamiwa na kundi la vijana wa kiume walioingia hotelini mahali mkutano huo ulipokuwa ukifanyikika. Hayo yameelezwa na Joseph Keitany kutoka polisi ya kaunti ya Kisumu. Mji wa Kisumu unafahamika kama ngome ya kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga.
Raila Odinga, Kiongozi wa upinzani Kenya (NASA)  
Vijana hao wavamizi wameiba komyuta mpakato na fedha za wanawake waliokuwa mkutanoni. Vijana hao wavamizi wamedai kuwa wanawake hao walikuwa wakinunua vitambulisho vya kupigia kura. Washiriki wa mkutano huo kwa upande wao wamekanusha madai hayo na kusema kuwa waliitisha mkutano wao ili kutafuta njia ya kushajiisha upigaji kura wa amani. Ripoti zinaeleza kuwa wanawake kadhaa walijeruhiwa katika hujuma na uvamizi uliofanywa na vijana hao.../

AYATULLAH MAKARIM SHIRAZI; NCHI ZA KIISLAMU ZIFUATILIYE MAUAJI YA WAISLAMU WA MYANMAR

Ayatullah Nasir Makarim Shirazi, mmoja wa Marjaa-Taqlidi wa hapa nchini ameeleza kusikitishwa na kimya cha Umoja wa Mataifa kuhusiana na mauaji ya Waislamu wa Myanmar na kusisitiza kwamba inapasa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu waitishe kikao cha haraka ili kusimamisha mauaji ya Waislamu hao madhulumu.
Akizungumza leo wakati wa darsa ya masomo ya juu kabisa ya fiqhi huko Qum kusini mwa Tehran, Ayatullah Makarim Shirazi ameongeza kuwa serikali ya Myanmar inapaswa iitishe kikao na maulamaa wa nchi za Kiislamu na kueleza sababu za mauaji ya kimbari yanayofanywa dhidi ya Waislamu.
Hapo jana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei naye pia alikosoa kimya cha jumuiya za kimataifa na wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kuhusiana na matukio ya maafa ya Myanmar na kusisitiza kwamba njia ya utatuzi wa kadhia ya Myanmar ni kuchukuliwa hatua za kivitendo na nchi za Kiislamu na kuishinikiza kisiasa na kiuchumi serikali isiyo na huruma ya nchi hiyo.
Waislamu madhulumu wa Myanmar
Wakati huohuo Ibrahim Rahimpour, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na eneo la Asia na Oceania ametangaza leo kuwa misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya Waislamu wa Myanmar itapelekwa nchini Bangladesh siku ya Ijumaa.
Akizungumza katika kikao cha dharura cha Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje Rahimpour ameongeza kuwa tani 100 za misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikijumuisha vifaa vya hospitali na madaktari bingwa kadhaa zitatumwa kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu wa Myanmar.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kwamba, mbali na hatua hiyo, mashauriano ya kisiasa yanaendelea kufanywa na serikali ya Myanmar na nchi jirani na nchi hiyo ili kuzuia mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu.
Wimbi jipya la mauaji ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa Myanmar lilianza tarehe 25 Agosti mwaka huu. Hadi hivi sasa maelfu ya Waislamu hao wameshauawa na kujeruhiwa na wengine karibu laki tatu wamekimbia makazi yao.../

Tuesday, September 12, 2017

UNYANYASAJI WATOTO WAKIMBIZI WA KIAFRIKA BARANI ULAYA

Katika hali ambayo, wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea barani Ulaya lingali linaendelea kushuhudiwa, ripoti za kimataifa zinaonyesha juu ya kuweko hali mbaya wanayokabiliwa nayo wahajiri hususan watoto wakimbizi wa Kiafrika.
Ripoti zilizotolewa na taasisi kadhaa za kimataifa zenye itibari zinaonyesha kuwa, watoto wahajiri wa Kiafrika wanaofanya jitihada za kuelekea barani Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa yakiwemo ya kufanyishwa kazi kwa nguvu, kupigwa na kutusiwa na kutumiwa vibaya kijinsia kuliko watoto wa maeneo mengine ya dunia waliolazimika kuhama makwao na kukimbilia nchi za Ulaya. 
Afshan Khan, Mkurugenzi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF kitengo cha Ulaya na Asia anaamini kuwa, kuna ukweli mchungu nao ni kwamba, watoto wahajiri wa Kiafrika wakati wanapovuka Bahari ya Mediterenia huwa wahanga wa unyanyasaji, magendo, kupigwa, kutusiwa na hata kubaguliwa na mambo hayo yamegeuka kuwa kitu cha kawaida.
Watoto wahajiri wa Kiafrika
Vita na mapigano ya ndani, machafuko ya kisiasa, mazingira mabaya ya kiuchumi ambayo yamefuatiwa na kupanda gharama za maisha, kutawala umasikini, ukosefu wa ajira, taathira ya mabadiliko ya tabianchi na kutokea janga la ukame katika baadhi ya nchi za Kiafrika na matokeo yake ni kuweko uhaba wa chakula ni mambo yanayotajwa kuwa sababu kuu ya wakazi wa nchi mbalimbali za Kiafrika kuamua kuhajiri na kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha mazuri.
Wengi wa wahajiri hao hupitia njia ya Libya na Bahari ya Mediterenia na kukumbana na hatari nyingi wakiwa katika juhudi za kufika katika mipaka ya nchi za Ulaya. Hii ni katika hali ambayo, kujikita magenge ya magendo ya binadamu katika pwani ya Libya na katika mipaka mingi ya nchi za Kiafrika na Ulaya ni jambo ambalo limeyafanya maisha ya wahajiri hao yawe hatarini na watoto wahajiri ndio wahanga wakuu.
Wahajiri wa Kiafrika wakiwa katika Bahari ya Mediterenia njiani kuelekea Ulaya
Kwa hiyo wahajiri hao ni chambo kizuri cha magenge ya magendo ya binadamu. Akthari ya wahajiri hao wamekuwa wakiuzwa na kununuliwa katika nchi mbalimbali na makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada kwa ajili ya kutumiwa katika operesheni za kigaidi na za kujitolea muhanga. Baadhi yao wamekuwa wahanga na viungo vyao kuuzwa.
Hata wale ambao hufanikiwa kuvuka na kukwepa hatari zote hizo na kuwasili barani Ulaya salama salmini, hujikuta wakikabiliwa na matatizo mengine kama unyanyasaji, kutumiwa vibaya kijinsia, kubaguliwa au kutumikishwa kwa nguvu. Yote hayo yanatokea katika hali ambayo, akthari ya nchi zimekuwa zikijigamba kuwa ni watetezi wa haki za watoto.
Licha ya kuwa viongozi wa nchi za Ulaya waliwaahidi viongozi wa Kiafrika kwamba, watatoa misaada ya kifedha na kusaidia kuboresha mwenendo wa ustawi barani Afrika kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wahajiri, lakini misaada yote hiyo, nayo imekuwa ni kwa ajili ya kudhamini maslahi ya nchi hizo za Ulaya badala ya kuzisadia nchi za Kiafrika.
Katika uwanja huo, mwishoni mwa mwaka 2015 Mfuko wa Dharura wa Dhamana wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Afrika ulianza shughuli zake kwa lengo la kufunga njia ya wimbi la wahajiri kuelekea barani Ulaya. Hata hivyo hivi sasa pamoja na kupita zaidi ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, utendaji wa mfuko huo wa dhamana nao umekuwa ukikabiliwa na ukosoaji.
Baadhi ya wahajiri wakiwa Ulaya 
Kiasi kwamba, asasi isiyo ya kiserikali inayojuliukana kama Action for Global Health (AfGH) imesisitiza katika moja ya ripoti zake kwamba, mfuko huo wa dharura wa dhamana wa Umoja wa Ulaya umeanzishwa ili kutoa majibu ya haraka kwa siasa za Ulaya na sio kwa ajili ya kutoa majibu kwa udharura wa ustawi katika nchi washirika. 
Katika mazingira kama haya inaonekana kuwa, kuangalia upya madola ya Magharibi siasa zao za kupenda vita, uingiliaji masuala ya nchi nyingine na ukoloni na vilevile kufanyika juhudi za kurejesha amani na uthabiti ni miongoni mwa mikakati ambayo asaa ikasaidia kupunguza wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya. Wakati huo huo, kuimarisha sheria na kuweko misaada kwa usalama na uzima wa kimwili na kiroho ni mambo ambayo kwa kiwango fulani yatarejesha usalama wa watoto.