Thursday, August 10, 2017

BUNGE LA MISRI LIMEZUIA POLISI KUTOTOA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Bunge la Misri Jumanne wiki hii limeidhinisha marekebisho ya sheria yanayowazuia askari polisi wa nchi hiyo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Marekebisho hayo ya sheria yanayohusiana na askari polisi ambayo yaliidhinishwa jana na bunge la Misri, yanawapiga marufuku polisi nchini humo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, kuchapisha nyaraka, ripoti au picha zinazohusiana na kazi zao bila ya kuwa na kibali cha maandishi.
Polisi yoyote atakayekiuka sheria hiyo mpya atakabiliwa na adhabu ya kifungo cha jela au kulipa fidia ya pauni za Misri elfu ishirini sawa na yuro 2026.
Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri mwezi Februari mwaka huu alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo achukue hatua za kubana mamlaka ya polisi nchini humo na pia awasilishe mapendekezo bungeni kuhusu suala hilo. Hii ni katika hali ambayo jumuiya za kutetea haki za binadamu na za mawakili nchini Misri kwa muda mrefu zimekuwa zikikosoa kile zinachokitaja kuwa ni kuwepo utamaduni wa kutoadhibiwa katika ngazi mbalimbali za utawala wa Misri; na kueleza kuwa, utumiaji mabavu na ukandamizaji wa polisi nchini humo umekuwa jambo la kawaida.
Mfano wa ukandamiza wa polisi ya Misri dhidi ya waandamanaji. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Wakati huo huo wakosoaji wa serikali ya Rais al Sisi wanaamini kuwa kupasishwa sheria hiyo mpya bungeni ni katika juhudi za kuficha maovu zaidi na vitendo vya ufisadi vinavyofanyika katika ngazi ya juu.

POLISI WANEE WAAUAWA MISRI KATIKA SHAMBULIZI LA DAESH ENEO LA SINAI

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daeh (ISIS) limekiri kutekeleza shambulizi dhidi ya gari la polisi ya Misri na kuua maafisa wanne wa usalama katika eneo la Sinai.
Shirika la habari la AMAQ limenukuu duru za usalama zikisema kuwa, genge hilo la kitakfiri ndilo lililohusika na hujuma ya jana Jumatano dhidi ya gari la kulinda doria la polisi ya Misri, katika mji wa al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.
Shambulizi hilo la Daesh linaonekana kuwa la ulipizaji kisiasa, ikizingatiwa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, wanachama wake 40 waliuawa baada ya vikosi vya usalama vya Misri kushambulia ngome zao katika Peninsula ya Sinai.
Gazeti la Al-Ahram la Misri limeripoti kuwa, magaidi hao waliliminia risasi gari hilo la doria na kuwaua maafisa wanne wa polisi waliukuwemo kwenye gari hilo na kwamba maafisa usalama tangu jana wamekuwa wakiwasaka kwa udi na uvumba wavamizi hao.
Wanachama wa Daesh katika eneo la Sinai nchini Misri
Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al-Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Eneo hilo halijawahi kushuhudia utulivu tangu magenge ya kigaidi yaanzishe harakati zao mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri. 

UPINZANI KENYA WAITAKA IEBC IMTANGAZE RAILA ODINGA MSHINDI WA UCHAGUZI WA URAIS

Mrengo wa upinzani wa NASA nchini Kenya umeitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC imtangaze mgombea wa muungano huo Raila Odinga kuwa, mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo siku ya Jumanne.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Nairobi hii leo kwa niaba ya muungano huo, Musalia Mudavadi, Wakala Mkuu wa NASA katika uchaguzi huo amesema, vyanzo vyao vya siri ndani ya IEBC vimewapa ithibati kuwa Odinga amepata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Uhuru Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili kupitia Chama cha Jubilee akipata kura milioni saba na laki saba. 
Mudavadi ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo amesema viongozi wa muungano huo wamefanya kikao na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mapema leo na kumkabidhi nyaraka za kuthibitisha madai yao.
Odinga (kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta
Hapo jana viongozi wa NASA walidai kuwa mfumo wa kupeperusha matokeo wa IEBC umedukuliwa, madai ambayo yalikanushwa vikali na maafisa wa tume hiyo.
Matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC yanaonesha kuwa, Kenyatta anaongoza kwa kura zaidi ya milioni 8, ambazo ni sawa na asilimia 53.89 ya kura zilizohesabiwa huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga akiwa na kura zaidi ya milioni sita na laki saba ambazo ni sawa na asilimia 44.47 ya kura.
Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imetangaza kuwa itatoa matokeo rasmi na ya mwisho ya kura za urais hapo kesho.

Tuesday, August 1, 2017

ZARIF: JAMII YA KIMATAIFA INAPASWA KUKOMESHA JINAI ZA ISRAEL

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, jamii ya kimataifa inalazimika kukomesha utamaduni wa kutouadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel na kuulazimisha utawala huo usitishe kabisa uhalifu na jinai zake dhidi ya watu wa Palestina.
Muhammad Javad Zarif ambaye jana jioni alikuwa akihutubia mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unaofanyika Istanbul nchini Uturuki kujadili kadhia ya Quds tukufu, amelaani mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na kusema kuwa: Umma wa Kiislamu unapaswa kusimama imara na kutomruhusu yeyote kuindoa jumuiya ya OIC katika malengo yake makuu ambayo ni kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu, kukomesha uvamizi wa Israel na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuunga mkono jitihada za kuundwa dola huru la Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.
Mkutano wa OIC, Istanbul
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa eneo la Ukanda wa Gaza na kusema, mzingiro huo ni jinamizi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linapaswa kushughulikiwa. Zarif amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umepuuza matakwa yote ya jamii ya kimataifa kwa ajili ya kusitisha na kubadili siasa zake za kibaguzi dhidi ya watu wa Palestina.
Tarehe 14 mwezi uliomalizika wa Julai Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia na kutoka katika Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa siku kadhaa, suala lililozusha machafuko makubwa na kupelekea kuuawa raia kadhaa wa Palestina.

KIONGOZI WA MASHAMBULIZI YA AL-SHABAD AANGAMIZWA SOMALIA

Wizara ya Habari ya Somalia imetangaza kuwa kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab anayehusika na suala la kupanga shambulizi ya kundi hilo ameangamizwa la jeshi la nchi hiyo.
Ali Mohammad Hussein maarufu kwa jina la 'Ali Jabal', alikuwa na jukumu la kuratibu na kutekeleza mashambulizi ya miripuko na mauaji nchini Somalia. Kadhalika Ali Jabal alikuwa akihusika na mashambulizi yaliyowalenga askari wa serikali katika eneo la Toro-toro, kusini mwa nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Wanachama wa genge la ash-Shabab

Hili ni shambulizi la pili la jeshi la Somalia kufanywa katika kipindi cha miezi miwili ya hivi karibuni ambapo idadi kubwa ya vinara wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai wameuawa. Kundi la kigaidi la ash-Shabab lililazimika kufungasha virago kutoka mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia mwezi Agosti mwaka 2011 baada ya kushadidi mashambulizi ya jeshi la serikali likishirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM. Hata hivyo genge hilo bado linadhibiti maeneo mbalimbali ya Somalia na linaendelea kufanya hujuma dhidi ya viongozi, askari na raia wa nchi hiyo.

Askari wa Umoja wa Afrika AMISOM

Katika fremu hiyo, Jumatatu ya jana jeshi la Uganda lilitangaza kuwa, askari 12 wa nchi hiyo wameuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi la al Shabab huko kusini mwa Somalia.

SYRIA NAYO YAIKOSOA SAUDIA KWA KUINGIZA SIASA KATIKA SUALA LA HIJJA

Serikali ya Syria imelalamikia vikali uendeshaji wa kisiasa wa ibada tukufu ya Hijja unaofanywa na utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Wizara ya Masuala ya Dini ya Syria imekosoa hatua ya Saudia ya kuwawekea vingiti raia wa Syria wanotaka kwenda kutekeleza nguzo hiyo ya Uislamu.
Taarifa hiyo iliyopeperushwa na shirika rasmi la habari la Syria SANA imeongeza kuwa, haki ya kwenda kuhijji inatumiwa kwa malengo ya kisiasa na utawala wa Riyadh.
Saudia ambayo haina uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Rais Bashar al-Assad, tangu mwaka 2012 imekuwa ikiwalazimisha raia wa Syria wanaotaka kwenda kufanya ibada ya Hijja kuomba viza katika nchi ya tatu, kupitia Kamati Kuu ya Hijja ya Syria, inayoongozwa na muungano wa kisiasa wa upinzani.
Mahujaji wakiwa wamefurika katika Mlima Arafa
Hii ni katika hali ambayo, awali Qatar pia ililalamika kuwa Riyadh imewawekea vikwazo na vizingiti chungu nzima Mahujaji wa Qatar wanaotaka kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu ya Uislamu mwak huu.
Kamisheni Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar imewasilisha malalamiko hayo kwa Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki ya kuabudu ikisisitiza kuwa kitendo hicho cha utawala wa kifalme wa Aal-Saudi cha kuendesha ibada ya Hija kisiasa kinakiuka sheria na makubaliano ya kimataifa yanayomdhaminia kila mtu uhuru wa kuabudu.
Huko nyuma Saudi Arabia imewahi kutumia ibada hiyo kisiasa dhidi ya Mahujaji wa Kiirani na Yemen. 

SAUDIA INATUMIA SILAHA ZA CANADA KUWAKANDAMIZA RAIA WAKE

Serikali ya Ottawa imesema inachunguza madai yaliyotolewa na vyombo vya habari na mashirika ya kiraia kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unatumia silaha zilizotengenezwa Canada katika ukandamizaji na jinai dhidi ya raia wake.
Upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Canada yameitaka serikali ya nchi hiyo isimamishe miamala na mauzo ya silaha kwa Saudia yakisisitiza kuwa Ottawa itajibebesha bure dhima ya ukatili unaofanywa na Riyadh dhidi ya raia wake wasio na ulinzi mashariki mwa nchi.
Vyombo vya habari nchini Canada vimesema kuwa, magari ya deraya na silaha zinazotumiwa na utawala wa Riyadh katika mashambulizi dhidi ya wakazi wa mashariki mwa nchi zina nembo za kuthibitisha kuwa zimetoka Canada.
Athari za hujuma za Aal-Saud dhidi ya wakazi wa al-Awamiya
Askari wa utawala wa kidikteta wa Aal-Saudi wameshadidisha mashambulizi kwa kutumia mizinga na silaha nyingine nzito katika makazi ya Waislamu wa Shia ya mji wa al-Awamiyah, mashariki mwa nchi hiyo.
Eneo la mashariki mwa Saudia limekuwa likishuhudia malalamiko ya wananchi wanaodai usawa tangu mwaka 2011. Hata hivyo badala ya utawala wa Aal-Saud kutekeleza matakwa ya wananchi, umekuwa ukitumia mkono wa chuma na ukatili kuwanyamazisha kwa nguvu wakazi wa mji wa al-Awamiyah.