Wednesday, April 12, 2017

SUDAN YAKIRI KUUAWA WANAJESHI WAKE NCHINI YEMEN

Duru mbalimbali za kijeshi za Sudan zimekiri kuwa wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo wameuawa nchini Yemen.
Televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imezinukuu duru za jeshi la Sudan zinazohusika na vita vya Yemen zikikiri kuwa wanajeshi watano wa nchi hiyo wameuawaa katika mapigano na jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, afisa mmoja wa kijeshi wa Sudan ni miongoni mwa wanajeshi waliouawa huko Yemen. Wanajeshi wengine 22 wa Sudan wamejeruhiwa.
Rais Omar al Bashir wa Sudan

Mwezi Februari 2016, Saudi Arabia ilitumbukiza dola bilioni moja katika Benki Kuu ya Sudan na kufanikiwa kubadilisha msimamo wa Rais Omar al Bashir aliyekubali kushirikiana na Saudi Arabia katika uvamizi na mauaji ya raia wa Yemen. Hata hivyo fedha hizo ni kama rehani na amana, wakati wowote Saudia itakapozihitajia, lazima Sudan izirejeshe. Imechukuliwa hatua hiyo ili kumbana Rais Omar al Bashir asibadilishe msimamo wake.
Vile vile Saudi Arabia imewekeza katika miradi ya maji safi nchini Sudan katika hatua nyingine inayoonekana ni kuwapa hongo Wasudan.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa, mgogoro wa Yemen ambao ulishadidi kutokana na uvamizi wa Saudi Arabia mwaka 2015, umeshapelekea maelfu ya raia wa kawaida kuuawa na miundombinu kuharibiwa kabisa.

Tuesday, April 11, 2017

BASI LA BORUSSIA DORTMUND LAKABILIWA NA MLIPUKO

Mechi hiyo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, Champions League, kati ya Borussia Dortmund na Monaco, ilikuwa ichezwe jana (11.04.2017) katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund.
Basi la timu ya Borussia Dortmund limeharibiwa na abiria mmoja kujeruhiwa baada ya milipuko mitatu kutokea karibu na basi hilo lililokuwa njiani kuelekea uwanja wa Signal Iduna Park umbali wa kiasi kilometa kumi ambako mechi ya ligi ya mabingwa, Chamiopns League, ilitarajiwa kuchezwa. Tukio hilo limetokea mwendo wa saa moja usiku saa za Ujerumani.
Msemaji wa jeshi la polisi katika jimbo la North Rhine Westphalia, Gunnar Wortmann, aliliambia shirika la habari la Associated Press, "Basi lilianza safari kutoka hoteli ya timu ya Dortmund wakati milipuko mitatu ilipotokea. Milipuko mitatu ilitokea karibu na basi hilo lilipokuwa njiani kuelekea uwanjani na kwamba mchezaji mmoja amejeruhiwa na dirisha moja kuharibiwa."
Beki wa Dortmund ajeruhiwa
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - FC Ingolstadt 04 Marc Bartra (picture-alliance) Beki wa Dortmund, Marc Bartra
Gazeti la Ujerumani la Bild limeripoti kwamba beki wa Borussia Doetmund Marc Bartra amejeruhiwa na kupelekwa hospitali. Klabu ya Dortmund imetuma taarifa katika mtandao wa kijamii wa Twitter ikisema mchezaji huyo yuko salama na hakuna kitisho chochote ndani na nje ya uwanja wa Signal Iduna Park.
Mkurugenzi wa klabu ya Dortmund, Hans-Joachim Watzke, alithibitisha kujeruhiwa kwa Bartra, akisema ameumia mkononi na kuwa majeruhi si hatari kwa maisha yake. 
Msemaji wa polisi ya Dortmund, Nina Vogt, alisema wachunguzi bado hawafahamu chanzo cha milipuko iliyotokea wakati timu ya Borussia Dortmund ilipokuwa ikijiandaa kuondoka hotelini kuelekea uwanjani kuchuana na Monaco. Polisi imesema inalichukulia tukio hilo kuwa shambulizi. Hata hivyo hakuna dalili kuonyesha ni shambulizi la kigaidi.
Explosion am BVB Bus (Reuters/K. Pfaffenbach) Basi la Borussia Dortmund likionekana hapa baada ya mlipuko karibu na hoteli ya timu hiyo kabla mechi
Dortmund iliamua kuiahirisha mechi hiyo ya duru ya kwanza ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya na kuutangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Twitter ikiongeza kuwa tiketi zote za mashabiki waliotaka kuutazama mtanange huo zinabaki kuwa halali na zitatumika leo.

KIONGOZI WA UPINZANI NCHINI ZAMBIA AKAMATWA NA POLISI

Polisi nchini Zambia imemtia mbaroni Hakainde Hichilema, kinara wa chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development.
Stephen Katuka, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha UPND ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, maafisa wa polisi walivamia makazi ya Hichilema na kumtia mbaroni bila kutoa maelezo yoyote kwa familia yake.
Katuka amekosoa vikali hatua ya polisi kumtia nguvuni kinara wa upinzani bila kutoa ufafanuzi wowote huku akitaja kama kitendo cha kinyama hatua ya polisi kuvamia makazi ya mwanasiasa huyo bila waranti na kisha kurusha mabomu ya kutoa machozi katika nyumba iliyokuwa na watoto wadogo.
Rais Edgar Lungu wa Zambia
Hata hivyo baadhi ya duru za usalama zimedokeza kuwa, Hichilema amekatwa kwa kuwa mwishoni mwa wiki alizuia msafara wa magari ya Rais Edgar Lungu, magharibi mwa nchi.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Oktoba mwaka jana, polisi ya Zambia iliwatia mbaroni Hichilema na Geoffrey Mwamba, Mkuu na Naibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development kwa tuhuma za uchochezi.
Uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi Agosti mwaka jana huko Zambia ulikuwa wenye ushindani mkali kati ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Edgar Lungu na mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema ambaye alidai kuibiwa kura.

Thursday, April 6, 2017

WAZAYUNI WAKIVAMIA TENA KIBLA CHA KWANZA CHA WAISLAMU

Karibu walowezi 50 wa Kizayuni leo Alkhamisi wamekivamia tena Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Masjidul Aqswa na kuuvujia heshima msikiti huo mtakatifu kwa ulinzi kamili wa polisi wa Israel.
Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina kimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, walowezi Wazayuni wameuvamia Msikiti wa al Aqsa kwa mara kadhaa katika kipindi cha wiki moja iliyopita na kuwashambulia walinzi wa eneo hilo takatifu.
Kwa mujibu wa kituo hicho cha habari, vitendo vya walowezi wa Kizayuni vya kuvamia Kibla cha Kwanza cha Waislamu vinazidi kuongezeka.
Mwezi Machi mwaka huu. walowezi 1,782 wa Kizayuni waliuvamia Msikiti wa al Aqsa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu ikiwa ni ongezeko la takriban mara mbili ikilinganishwa na mwezi Machi mwaka jana ambapo walowezi 960 walilivamia eneo hilo tukufu.
Masjidul Aqswa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Mwezi Machi mwaka huu pia, taasisi zenye misimamo mikali za Kiyahudi zilitoa mwito mara kadhaa wa kuvamiwa na Wazayuni, Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Masjidul Aqswa imegeuzwa kuwa eneo la kuonesha jeuri za wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni wenye nia ya kuupokonya msikiti huo sura na utambulisho wake wa Kiislamu.
Kuwepo msikiti huo mtakatifu na maeneo mengine matukufu kwa Waislamu na Wakristo, kunaufanya mji wa Baytul Muqaddas huko Palestina kuwa eneo takatifu kwa wafuasi wa dini hizo mbili.
Hata hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya njama za kila namna za kuuyahudisha mji huo na kuupokonya kabisa sura yake ya Kiislamu na pia ya Kikristo.

Saturday, April 1, 2017

ICC YATAHADHARISHA KUHUSU UKATILI UNAOFANYIKA CONGO DR

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetahadharisha kuwa ukatili uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa unaweza kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita.
Taarifa hiyo ya mahakama ya ICC imetolewa baada ya mauaji ya karibu watu 400 wakiwemo wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden katika mkoa wa katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wa Kasai.  
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Fatou Bensouda amesema kuwa, amepokea ripoti kuhusu ukatili unaofanyika katika mapigano yamayojiri kati ya makundi ya wanamgambo na jeshi la serikali ya Congo, mauaji ya idadi kubwa ya raia, utekaji nyara na kunyongwa ovyo watu wasio na hatia. Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweza kutambuliwa kuwa ni jinai za kivita. 
Raia wengi wanaoawa Kasai, Congo
Bensouda amesisitiza kuwa hatasita kuwachukulia hatua na kuwapandisha kizimbani watu wanaohusika na uhalifu huo. 
Mkoa wa Kasai umekumbwa na ghasia tangu katikati ya mwezi Agosti, wakati askari wa kikosi cha serikali ya Congo walipomuua Kamwina Nsapu, aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo waasi dhidi serikali kuu Rais Joseph Kabila.
Wiki iliyopita pia wanamgambo wa eneo hilo waliwaua kwa kuwakata vichwa maafisa karibu 40 wa jeshi la polisi ya nchi hiyo katika maeneo ya msituni mkoani Kasai.

UHUSIANO WA SAUDIA NA SUDAN, HAKIKA AU MASLAHI YA MUDA?

Saudi Arabia inafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Sudan yajulikanayo kama 'Ngao ya Samawati -1' huku nchi hizo mbili zikijaribu kuimarisha uhusiano wao kutokana na vizingiti vya ndani ya nchi na kieneo.
Mazoezi hayo ya anga baina ya majeshi ya Sudan na Saudia yanayofanyika katika mipaka ya kaskazini mwa Sudan, yameanza Machi 29 na yataendelea hadi Aprili 12.
Uhusiano wa Sudan na Saudi Arabia umekuwa ukiimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Sudan ni kati ya nchi ambazo zinashiriki katika hujuma ya kinyama ya Saudia nchini Yemen. Pamoja na hayo, ushiriki wa Sudan katika muungano huo wa Saudia, sawa na ushiriki wa nchi zinginezo, ni wa kinembo tu na kwa ajili ya kupata misaada ya kifedha ya Saudia.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa Sudan na Saudia wamekuwa wakikutana kujadili uhusiano wa pande mbili katika sekta za kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Ingawa Sudan inataka misaada ya kifedha katika uhusiano wake na Saudia, lakini mkondo wa kuimarika uhusiano wao ni katika fremu ya Saudi Arabia kutaka kujipenyeza na kuwa na ushawishi barani Afrika. Ni kwa msingi huo ndio maana Rais Omar El Bashir wa Sudan hivi karibuni akatoa matamshi ya kustaajabisha kuwa eti usalama wa Saudia ni usalama wa Sudan!
Ndege ya kivita ya Saudia
Sababu kuu ya Saudia kukodolea macho ya tamaa nchi za Afrika ikiwemo Sudan ni matukio ya kasi Mashariki ya Kati ambayo hayaendi tena kwa maslahi ya watawala wa Riyadh. Wakuu wa Saudia wanaamini kuwa, hivi sasa uwezo na satwa yao iko katika mkondo wa kuporomoka katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa msingi huo,  Saudia sasa inataka kutumia uwezo wake wa kifedha ili kueneza ushawishi wake ya kisiasa barani Afrika na kupata waitifaki katika bara hilo. Kwa msingi huo,  Sudan imesema Saudia itawekeza dola bilioni 111 nchini Sudan na kwamba kiwango hicho cha uwekezaji kitaongozeka maradufu katika siku za usoni.
Wakati huo huo, Saudi Arabia kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika nchi za Kiarabu na Kiafrika inataka kutuma ujumbe huu kwa nchi zingine kuwa ina ushawishi mkubwa katika katika nchi za Kiafrika na Kiarabu.
Eneo la Hala'ib la Sudan kaskazini linalozozaniwa na Misri
Weledi wa mambo wanasema hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Saudia kufanya mazoezi ya kijeshi na Sudan, wakuu wa Riyadh wanataka kutuma ujumbe kwa nchi jirani ya Misri. Hii ni kwa sababu mazoezi hayo yanafanyika karibu na mpaka wa Sudan na Misri wakati uhusiano wa Misri na Saudia unaripotiwa kuvurugika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Nukta muhimu hapa ni kuwa, licha ya mazoezi hayo ya kijeshi, uhusiano wa Sudan na Saudia unaimarika kwa sababu ya matatizo yaliyoibuka hivi sasa katika nchi hizo mbili. Katika upande mmoja Saudia inashuhudia kufeli sera zake zisizo na busara Mashariki ya Kati huku serikali ya Omar El Bashir nayo ikikumbwa na matatizo mengie ya kiuchumi na hivyo kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya wananchi.

RAIS WA TUNISIA: IRAN NDIYO TEGEMEO PEKEE KWA AJILI YA KUKABILIANA NA ISRAEL

Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amesema kuwa Iran ndio tegemeo pekee kwa ajili ya kukabiliana na Israel.
Rais wa Tunisia ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Utamaduni wa Iran aliyeko nchini humo na kuongeza kuwa, adui mkubwa zaidi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati ni utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba anatarajia nchi zote za Kiislamu na Kiarabu zitakuwa bega kwa bega na Iran katika suala hilo.
Beji Caid Essebsi amesema utawala wa Kizayuni na washirika wake wanafanya jitihada za kuitenga Jamhuri ya Kiislamu lakini njama hizo zimegonga mwamba. Amesisitiza kuwa, Iran ni nchi kubwa na yenye utamaduni tajiri na kwa msingi huo inapaswa kutekeleza majukumu yake katika eneo la Mashariki ya Kati. 
Rais wa Tunisia, Beji Caid Essebsi 
Rais wa Tunisia amesema kuwa nchi yake haitaathirika na misimamo ya nchi nyingine katika uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 
Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni ya Miongozo ya Kiislamu wa Iran, Ridha Salehi Amiri amesifu uhusiano mzuri wa kiutamaduni, kiuchumi na kibiashara wa Iran na Tunisia.
Ameashiria hali ya sasa ya Mashariki ya Kati na kusema: Hali ya eneo hilo imebadilika sana baada ya matukio ya Iraq na Syria na kuongeza kuwa: Kama si mapambano ya Iran dhidi ya magaidi waliovamia nchi hizo hii leo magaidi wangekuwa katika miji ya Baghdad na Damascus na kirusi hicho kingezikumba nchi nyingine za Waislamu.